RAIS SAMIA APONGEZA GAWIO ATAKA BIDII ZAIDI
RAIS
Samia Suluhu Hassan amepongeza taasisi na kampuni za umma zilizotoa gawio la Sh
trilioni 1.327 na kuagiza zisibweteke.
Akizungumza
kwenye hafla ya Siku ya Gawio Ikulu Dar es Salaam leo, Rais Samia alisema
gawio hilo limetokana na uzalishaji na kuimarika kwa tija na ufanisi wa taasisi
hizo.
Siku
ya Gawio ni jukwaa la kuwapa wananchi fursa ya kuona matokeo ya uwekezaji
unaofanywa kwa niaba yao. Kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, takribani
taasisi na kampuni za umma 308 zinatakiwa kutoa gawio kwa serikali ambayo mpaka
Juni 2025, imewekeza zaidi ya Sh trilioni 92 katika taasisi na kampuni za umma.
Rais
Samia alisema anatarajia gawio kubwa zaidi mwakani na atafurahi ikiwa hivyo.
Ameonya watumishi wazembe na wenye matumizi mabaya ya rasilimali za nchi kwamba
hawatasita kuwachukulia hatua.
“Mwaka
huu tumepata Shilingi trilioni 1. 327 kulinganisha na Shilingi trilioni 1.028
za mwaka jana, tumeongeza karibu Shilingi bilioni 300 si haba, mambo sio
mabaya. Nawapongeza wote mliochangia mafanikio haya lakini msibweteke…
Najivunia ninyi,” alisema rais.
Aliongeza:
“Tathmini hii niliagiza mwaka jana ifanyike na Msajili wa Hazina (Nehemiah
Mchechu) na timu yake waliifanya vizuri na matokeo yake tumeyaona… Wote
wametuonesha kuwa taasisi za umma zinaweza kufanya vizuri kwa kutoa huduma na
kujiendesha kwa ufanisi kushindana katika mapato ya serikali, haya ndio maono
na mwelekeko tunaotaka kwa hiyo kwenye mafanikio hatuatacha kuwatambua,”
alisema.
Alisema
huo ndio mwelekeo inaoutaka serikali na pongezi zake ziwe chanzo cha kuongeza
juhudi na maarifa, kwani gawio ni sehemu ya lengo la serikali la kuongeza
mapato ya ndani.
“Tulipotoka
ni mbali, tunakwenda polepole. Bajeti ya mwaka huu, kipande cha kujitegemea
kimebaki kidogo, tukikaza mwendo baada ya miaka miwili tutakwenda vizuri,”
alisema.
Kuhusu
kufanyika kwa mageuzi katika taasisi, alisema alielekeza kwenye hafla za mwaka
jana kwamba taasisi hizo haziwezi kutegemea serikali kwa kila changamoto wakati
zina uwezo.
Alisema
sasa zimeanza kuonekana, huku akitolea mfano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA), kwamba ina uwezo wa kukopa fedha ikatanua bandari, wakawa na uwezo wa
kulipa mkopo wenyewe.
Rais
Samia alitoa maelekezo kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuendelea na kazi ya
kutathmini taasisi hizo na ipewe uzito unaostahili, lengo likiwa ni kutoka
kwenye dhamira na kufikia malengo waliyojiwekea.
Akizungumzia
kaulimbiu ya Siku ya Gawio: “Uwekezaji wa Umma wenye Matokeo: Nguzo ya Uchumi
Shindani na Maendeleo Endelevu Kuelekea Dira 2050,” rais alisema inakumbusha
uwekezaji wenye matokeo ni unaovutia mitaji, kupunguza gharama za kufanya
biashara, kukuza huduma, kuongeza mapato ya serikali na kulinda maslahi ya
wananchi.
“Ili
kaulimbiu hiyo ipate maana na uhalisia lazima itafsiriwe katika misingi ya kazi
na huduma kwa wananchi ili tufikishe huduma na kukuza uchumi wetu. Nasisitiza
sababu utekelezaji wa dira unahitaji taasisi zenye uwezo wa kuingia kwenye
ushindani wa soko,” alisema.
Aliongeza:
“Tunapoianza kesho (leo) kutumia dira, tunatakiwa kuwa makini, taasisi zetu
ziwe imara kwelikweli, wenye taasisi zenye kichefuchefu (zisizofanya vizuri)
zitafutiwe dawa zitulie ili twende nazo pamoja.”
Rais
Samia alizitaka taasisi hizo kufungua milango kwa sekta binafsi, akisisitiza
kwamba hataki taasisi zinazofanya kazi kwa mazoea. Alisema ili nchi ijenge
uchumi shindani, inahitaji taasisi zinazoleta matokeo ili kutoka kwenye takwimu
na kwenda kwenye ukweli.
“Tunasema
mipango sio matumizi. Maofisini mwetu tuna mipango mingi, sera, mikakati, kauli
kabambe lakini zipo tu, hayo si matumizi. Dira yetu nzuri sana, ndani yake tuna
mipango ya maendeleo ya muda mfupi na mrefu na tumemaliza nyenzo zinazoongoza
utekelezaji wake lakini yote hayo hayataleta maendeleo ya nchi kama hakuna
kutafsiri, kutathmini na kusimamia utekelezaji wake. Kwa hiyo tujipange kwenye
utekelezaji wa dira yetu,” alisema.
“Msajili
wa hazina, kampuni, taasisi za serikali na Watanzania wote, twende tukaitafsiri
na kutekeleza dira yetu kila mmoja katika maeneo tofauti tofauti,” alisema
rais.
Alizitaka
wizara kusimamia taasisi zake na kutafsiri dira kwenye mpangokazi wao, akisema
hilo si jukumu la msajili pekee.
Wakati
huo huo, Rais Samia pia alikabidhiwa tuzo kwa kutambua mchango wake kwenye
mafanikio hayo. Alisema ameipokea kwa unyenyekevu, akitambua ni ya kazi ya
pamoja na si peke yake.


Post a Comment