Chakwera,Tume ya Jaji Chande wateta



Rais Mstaafu wa Malawi, Mhe. Lazarus Chakwera ambaye ni Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Shirley Ayorkor Botchwey, amefanya mazungumzo na Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Mkutano huo ulifanyika Aprili 11,2026 katika Jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Jijini Dar es Salaam. 

Chakwera amesema ujumbe wake umekuja Tanzania lengo kuu likiwa ni kutafuta suluhisho la kutafuta Suluhu la Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

“Ujumbe wangu umekuja Tanzania kwa lengo la kila mmoja kutafuta Suluhu ya yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi hilo ndilo muhimu kwa sasa mengine nitazungumza baada ya kuhitimisha ziara yangu ya Tanzania,” amesema Chakwera.

Akizungumzia ziara hiyo, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Othuman Chande, alisema mazungumzo yao yalijikita zaidi kueleza shughuli za Tume hiyo na hadidu za rejea za Tume huku akiwataka waandishi kusubiri taarifa za mjumbe huyo baada ya kukamilisha ziara yake nchini Tanzania. 

Mjumbe huyo jana alikutana na Msajili wa Vyama vya Siasa na viongozi wa vyama mbalimbali. Bado anaendelea na ziara yake ya kikazi ambayo anataraji kuhitimisha Aprili 16,2026 baada ya kutembelea Zanzibar na Dodoma.Rais huyo wa zamani tayari ameshakutana na ujumbe wa Serikali ya Tanzania ukingozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi na kujadiliana kuhusu namna Tanzania ilivyojidhatiti katika kudumisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Kikao hicho kilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyrere (JNICC) siku ya Alhamisi Aprili 9, 2026 Mhe. Profesa Kabudi alimueleza kwa kina Mjumbe huyo Maalum, kuhusu hatua mbalimbali zinazoendelea kuchululiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuimarisha demokrasia nchini huku ikiweka msisitizo katika kulinda na kuheshimu utu wa Mtanzania, kuzingatia haki na uwajibikaji, amani na utulivu pamoja na kudumisha umoja wa kitaifa.

Mbali na kukutana na ujumbe wa Serikali, Mheshimiwa Chakwera anatarajiwa kukutana na wadau mbalimbali ambapo jana Aprili 10, 2026 alikutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. Jaji Mstaafu Francis Mutungi pamoja na vyama vya siasa vya ACT–Wazalendo, Chama cha National League for Democracy (NLD), United Democratic Party (UDP), Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Chama cha NCCR Mageuzi, Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Alliance for African Farmers Party (AAFP) na Chama cha ADA-TADEA.

Vyama vingine ni pamoja na Democratic Party (DP), Tanzania Labour Party (TLP), Union for Multiparty Democracy (UMD), United People’s Democratic Party (UPDP), Chama cha Kijamii (CCK), Demokrasia Makini, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Akiwa nchini Mheshimiwa Chakwera anatarajia pia kukutana Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jaji Joseph Warioba, Jumuiya zisizo za Kiserikali, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Mhe. Jaji George Joseph Kazi, Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Mhe. Othman Masoud Othman, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jaji George Mcheche Masaju, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Mhe. Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro.

Aidha, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, atakutana pia na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



No comments