RAIS DKT. SAMIA AZIDI KUNG’ARA KIMATAIFA, ATUNUKIWA SHAHADA YA HESHIMA NIGERIA




RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezidi kujiimarisha katika medani ya kimataifa baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi (Doctor of Letters – Honoris Causa) kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Nasarawa nchini Nigeria.

Tukio hilo la kihistoria limefanyika leo katika Mahafali ya Nane ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye kampasi ya Keffi nchini humo, ambapo Rais Dkt. Samia alishiriki na kupokea heshima hiyo kwa njia ya mtandao akiwa Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Chuo hicho kimetoa tuzo hiyo kama alama ya kutambua uongozi wa mageuzi wa Rais Dkt. Samia unaojali uwazi na uwajibikaji. Aidha, chuo hicho kimeguswa na jitihada zake katika kukuza uchumi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, na mapinduzi anayoyafanya katika kuwawezesha wanawake na vijana, hususan kupitia fursa za Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).

Pia, juhudi za Rais Dkt. Samia katika kusimamia afya ya mama na mtoto pamoja na kampeni yake ya matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika, zimetajwa kuwa miongoni mwa sifa zilizompa heshima hiyo ya juu.




Rais Dkt. Samia ameweka rekodi nyingine kwa kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya kigeni nje ya Nigeria kutunukiwa shahada ya heshima na chuo hicho, akijiunga na watu mashuhuri kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, na tajiri namba moja barani Afrika, Aliko Dangote.

Akizungumza baada ya kutunukiwa, Rais Dkt. Samia amesema amepokea tuzo hiyo kwa unyenyekevu na kusisitiza kuwa ni heshima kwa Watanzania wote wanaopambana kuleta maendeleo barani Afrika.

“Napokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa. Tuzo hii si yangu pekee, bali inaakisi jitihada za pamoja za wananchi wa Tanzania katika kuendeleza maendeleo, ushirikiano na ustawi wa Bara la Afrika,” alisema Rais.

Katika kuitumia fursa hiyo kimkakati, Rais Dkt. Samia ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuanza mazungumzo na chuo hicho ili kuanzisha ushirikiano wa kitaaluma, ubadilishaji wa wanafunzi na tafiti za pamoja kati ya Tanzania na Nigeria.

Chuo Kikuu cha Jimbo la Nasarawa kinatajwa kuwa miongoni mwa vyuo bora nchini Nigeria kikishika nafasi ya nane kati ya vyuo 309 nchini humo, huku kikiwa katika nafasi ya 36 kwa ubora katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

No comments