SANAA YA USUSI: MKOMBOZI WA KIUCHUMI KWA VIJANA TANZANIA
![]() |
| Rose Mkoyi |
Katika ulimwengu wa sasa ambapo ushindani wa soko la ajira rasmi umekuwa changamoto kubwa, sanaa ya urembaji na ususi imeibuka kuwa moja ya sekta zinazokua kwa kasi nchini. Sekta hiyo si tu kielelezo cha urembo, bali ni injini ya kiuchumi inayotoa fursa za kipato cha haraka na endelevu kwa vijana walioamua kutumia vipaji vyao na ujuzi wa amali kujikwamua kimaisha kupitia ubunifu wa hali ya juu na ufundi wa mikono.
Simulizi ya binti mjasiriamali Rose Mkoyi ni kielelezo tosha cha jinsi sanaa inavyoweza kuvuta ndoto za vijana kutoka pembe mbalimbali za nchi, ambapo alifunga safari ndefu kutoka mkoani Simiyu hadi Kisesa mkoani Mwanza akisaka ujuzi. Rose, ambaye sasa ni mwanafunzi katika Chuo cha Pine, anaamini kuwa fani hiyo si kuhusu kupamba watu pekee, bali ni ufundi unaohitaji weledi wa hali ya juu ili kuleta matokeo yanayogusa hisia za mteja na kumjengea sifa ya kuwa mbunifu mkubwa wa mitindo nchini.
Uwepo wa vyuo kama Pine mkoani Mwanza umekuwa chemchemi ya ujuzi kwa kutoa mafunzo ya amali yanayogusa mahitaji halisi ya soko, ikiwemo ususi, urembaji, na fani nyingine kama ujenzi. Taasisi hizi zinalenga kuzalisha nguvukazi iliyokamilika inayoweza kutoisubiri ajira bali kuitengeneza wenyewe, jambo linalompa kijana ujasiri wa kusimama imara kiuchumi kwa kutumia mtaji mdogo na vifaa vya msingi kuanza kutoa huduma hata akiwa nyumbani.
Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), likiwa mlezi mkuu wa sanaa nchini, linasisitiza umuhimu wa wasusi na mafundi urembo kujisajili na kutambulika rasmi ili kulinda kazi zao na kupata fursa za kukuza vipaji. Basata inatambua kuwa ususi ni sehemu ya sanaa za ufundi zinazobeba utamaduni na utambulisho wa Mtanzania, huku ikibainisha kuwa msanii aliyesajiliwa anakuwa na nafasi nzuri ya kupata mikopo, masoko, na hata kushiriki katika mashindano ya kimataifa.
Uamuzi wa vijana kama Rose kujiendeleza kitalaamu ndio ufunguo wa milango ya mafanikio, kwani ujuzi wa mikono haufi wala kupoteia bali huongezeka thamani kadiri muda unavyoenda. Ni wito kwa jamii na wazazi kuwahimiza vijana kujiunga na vyuo vya ufundi ili wapate silaha ya maisha, huku sekta ya urembo ikiendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mzunguko wa fedha mitaani na kutoa heshima kwa fani za ufundi nchini Tanzania.

Post a Comment