KUTOKA TUNISIA HADI BOTSWANA: SERENGETI GIRLS KUHITIMISHA KAMBI LEO

 



Na Zena Chande, Monastir

TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Girls, leo inashuka dimbani kumenyana na wenyeji wao, Tunisia, katika mchezo wa pili wa kirafiki wa kimataifa utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mustapha Ben Jannet mjini Monastir. 

Mchezo huo ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya kikosi hicho kuelekea mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zilizopangwa kufanyika nchini Morocco baadaye mwaka huu.

Katika mchezo wa kwanza wa kujipima nguvu uliopita, Serengeti Girls ilionyesha cheche zake kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Tunisia, matokeo yaliyoongeza hali ya kujiamini kikosini. 

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime, ameeleza kuwa ana imani kubwa ya kupata matokeo mazuri zaidi leo, akibainisha kuwa wachezaji wake sasa wamezoea hali ya hewa ya baridi kali iliyopo nchini humo tofauti na walivyowasili wiki moja iliyopita.

"Tulikuta baridi kali sana huku, lakini tulifanikiwa kushinda mechi ya kwanza siku chache tu baada ya kuwasili. Sasa tumekaa hapa Monastir kwa takriban siku saba, wachezaji wamezoea mazingira na kikosi kipo vizuri kiushindani," alisema Shime. Aliongeza kuwa kambi hiyo nchini Tunisia imekuwa na tija kubwa katika kukiimarisha kikosi chake kiufundi na kisaikolojia kabla ya kuanza safari ya mashindano rasmi.



Mara baada ya mchezo wa leo, Serengeti Girls inatarajiwa kuhitimisha kambi yake nchini humo na kesho kuanza safari ya kuelekea Francistown, Botswana, kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa kufuzu Kombe la Dunia. 

Endapo itafanikiwa kuiondoa Botswana, Serengeti Girls itakutana na Afrika Kusini katika hatua inayofuata, ikisaka nafasi ya kurejea kwenye mashindano hayo makubwa ambapo mwaka 2022 iliweka historia ya kufuzu fainali zilizofanyika nchini India.

No comments