RAIS SAMIA AFANYA UTEUZI NA KUFANYA MABADILIKO MADOGO BARAZA LA MAWAZIRI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi, uhamisho na utenguzi wa viongozi mbalimbali katika Baraza la Mawaziri, Bunge na taasisi za kiserikali ili kuongeza ufanisi katika utendaji.
Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa Aprili 2, 2026, Rais amemteua Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, akitokea Ofisi ya Rais Ikulu ambako alikuwa Waziri wa Nchi (Kazi Maalum).
Katika hatua nyingine, Rais amemhamisha Mhe. Reuben Nhamanilo Kwagilwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) na kumteua kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Wakati huo huo, Mhe. Dkt. Festo John Dugange amehamishwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) anayeshughulikia Masuala ya Elimu. Aidha, Balozi Ali Jabir Mwadini ameteuliwa kuwa Katibu wa Rais.
Rais Samia pia ametumia mamlaka yake kuteua wabunge wapya wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo amewateua Dkt. Eveline Wilbard Munisi na Bi. Angela Kizigha kushika nyadhifa hizo.
Katika sekta ya diplomasia, Balozi Said Othman Yakub amepangiwa kituo kipya cha kazi ambapo ataiwakilisha Tanzania nchini Ufaransa kama Balozi.
Pamoja na uteuzi huo, Rais amefanya utenguzi wa uteuzi wa Dkt. James Andilile Mwainyekule, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Bakari S. Machumu, imebainisha kuwa Dkt. Mwainyekule atapangiwa majukumu mengine. Hafla ya uapisho kwa Waziri na Naibu Mawaziri wateule inatarajiwa kufanyika katika tarehe itakayopangwa baadaye.
Post a Comment