Mwanadamu arejea mwezini:Ratiba ya Kila Siku ya Wanaanga wa Artemis kuuzunguka

 


 

Safari ya siku 10 ya Artemis 2 ya NASA inajawa na tafiti za kisayansi, majaribio ya chombo, uchunguzi wa afya, mafunzo ya kujiokoa na mengine mengi.

Artemis 2 ya NASA inasafirisha wanaanga wanne katika safari ya siku 10 kuzunguka mwezi.

Wafanyakazi hao watakuwa ndani ya chombo cha Orion, wakitekeleza malengo mengi yakiwemo safari ya kwanza ya binadamu kupita karibu na mwezi katika kipindi cha zaidi ya nusu karne.

Wanaanga hao watatumia takriban saa tatu katika eneo la karibu zaidi na mwezi, na kila dakika ya safari yao imepangwa kwa umakini.

Wanaanga hao Reid Wiseman, Victor Glover, na Christina Koch (NASA), pamoja na Jeremy Hansen (Shirika la Anga la Kanada) wanatarajia kuleta utaalamu mpya kuhusiana na mwenendo wa safai na jinsi mwezi unavyoonekana.

Mchanganuo wa ratiba yao ya kila siku uko hivi:



Siku ya Urushaji Aprili 2 (Launch Day)

Dakika nane za kwanza ni  muhimu zaidi. Wanaanga watarushwa na roketi ya Space Launch System (SLS). Baada ya kufika angani, chombo cha Orion kitatengana na roketi na kuanza mfululizo wa majaribio.

Majaribio ya Ukaribu (Proximity Operations): Wanaanga wataendesha Orion kuzunguka sehemu ya roketi iliyotumika (ICPS) ili kudhihirisha uwezo wa Orion wa kuruka karibu na vitu vingine angani. Baada ya hapo, wataanza ukaguzi wa mifumo, kuvua suti zao za anga na kuvaa nguo za kawaida kabla ya kulala kwa saa 8.5.

Siku ya 2: Mazoezi

NASA imeweka vifaa vya mazoezi ndani ya Orion ili kupunguza athari za hali ya kutokuwa na uzito (microgravity) mwilini.

Translunar Injection (TLI): Saa sita baada ya kuamka, wanaanga watafanya manuva ya TLI. Huu ni muungurumo wa injini kwa dakika 30 utakaokisukuma chombo kuelekea mwezini. Bila hatua hii, chombo kitabaki kuzunguka dunia pekee.

Siku ya 3: Mapigo ya Moyo na Uchunguzi wa Mwezi

Wakiwa njiani kuelekea mwezini, wanaanga watatumia siku hii ya tatu kufanyia mazoezi kazi watakazozifanya watakapofika karibu na mwezi. Ni muhimu kuzoea kufanya kazi hizi katika hali ya kutokuwa na uzito. Pia, watafanya mazoezi ya usalama, ikiwemo huduma ya kwanza ya mapigo ya moyo (CPR) angani.

Siku ya 4: Picha za Dunia na Mwezi

Siku ya nne Orion itafanya marekebisho madogo ya njia. Wanaanga watatumia muda mwingi kuwasiliana na kituo cha udhibiti duniani na kufanya mazoezi ya kutumia darubini. Dakika 20 zimetengwa mahususi kwa ajili ya kupiga picha za Dunia na Mwezi wakiwa katikati ya safari.

Siku ya 5: Kuingia Katika Eneo la Mwezi

Hii ndiyo siku ambayo nguvu ya mvutano ya mwezi inakuwa na nguvu zaidi kuliko ya Dunia kwa chombo cha Orion.

Wanaanga watafanya majaribio ya kuvaa suti zao za anga kwa haraka (donning test) ili kujiandaa na dharura yoyote ya kupotea kwa hewa ndani ya chombo.


Siku ya 6: Kupita Karibu na Mwezi (Lunar Flyby)

Hii ndiyo siku kuu ya shughuli yenyewe! Wanaanga watapita umbali wa maili 4,000 hadi 6,000 (kilomita 6,440 - 9,650) juu ya uso wa mwezi. Kwa wanaanga hao, mwezi utaonekana mkubwa kama mpira wa kikapu ulio karibu. Watatumia saa tatu kuchukua data, kupiga picha, na kuchunguza maumbo ya kijiolojia.

Siku ya 7: Kurudi Duniani na Mawasiliano na ISS

Siku ya saba ya safari Orion itaanza taratibu za kurejea duniani. Wanaanga watatuma data kwa wanasayansi duniani kuhusu utendaji wa chombo na hali zao za kisaikolojia.

 Pia, kutakuwa na tukio la kihistoria: mazungumzo ya sauti kati ya wanaanga wa Orion na wale waliopo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS).

Siku ya 8: Kinga dhidi ya Mionzi na Manuva

Kinga ya Mionzi: Ili kujilinda na mionzi ya jua, wanaanga watatumia matangi ya maji ya chombo hicho kama ngao ya kujikinga na mionzi upande mmoja.

Udhibiti wa Mkao (Attitude Control): Watafanya majaribio ya uendeshaji wa chombo kwa kutumia mifumo tofauti ya injini ili kuona jinsi chombo kinavyoweza kugeuka bila kupoteza njia yake.

Siku ya 9: Maandalizi ya Mwisho

Wanaanga wataanza kufunga kila kitu na kujiandaa kwa ajili ya kutua. Watavaa nguo maalum za kubana (compression garments) zinazosaidia mwili kuhimili mabadiliko ya shinikizo utakapofika duniani baada ya kukaa muda mrefu bila uzito.

Siku ya 10: Kuingia Kwenye Anga la Dunia na Kutua Baharini

Hii ndiyo hatua ya mwisho yenye joto kali. Orion itatenganisha sehemu yake ya huduma (service module) na kuelekeza ngao ya joto kuelekea mbele. Ngao hiyo itawalinda na joto la nyuzi joto 1,650 Celsius wakati wakipita kwenye anga la Dunia.

Miamvuli mitatu itafunguka ili kupunguza kasi, na chombo kitatua kwenye Bahari ya Pasifiki, karibu na pwani ya San Francisco, ambapo meli ya Jeshi la Majini la Marekani itawapokea na kuhitimisha safari hiyo.

 

No comments