SERIKALI YAPANUA WIGO WA MAFUNZO NA FURSA ZA AJIRA KUINUA USHINDANI WA NGUVUKAZI YA WATANZANIA KATIKA SOKO LA KIMATAIFA



Katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya kasi ya kiuchumi na kiteknolojia duniani, Serikali imeweka mkazo wa kipekee katika kuimarisha ujuzi wa nguvukazi ya ndani na kupanua wigo wa fursa za ajira ili kuwajengea Watanzania uwezo wa kushindana vyema katika soko la ndani na nje ya nchi. 

Akisoma Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2026/2027 jijini Dodoma, Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amebainisha kuwa juhudi hizi ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya vitendo inayolenga kuzalisha ajira zenye tija na kuinua viwango vya utaalamu kwa wananchi wote. 

Serikali imekuwa ikiratibu kwa karibu utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ili kubaini na kuzalisha nafasi mpya za kazi, huku ikijenga mazingira rafiki kwa wawekezaji na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, hatua inayolenga kuhakikisha kunakuwepo na ajira zenye staha na endelevu kwa vijana.

Katika kuelekea kilele cha mafanikio ya kuimarisha ujuzi, Serikali imefanikisha mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 5,746 kupitia vyuo na taasisi 46 katika kipindi cha mwaka 2025/2026, sambamba na kutoa mafunzo maalum kwa wakulima na wasindikaji wadogo 1,065 ili kuongeza thamani ya mazao na kupunguza upotevu wa malighafi. 

Taarifa ya Waziri MkuuDkt. Mwigulu Nchemba inaonesha kuwa hadi kufikia Februari 2026, jumla ya ajira 625,273 zilikuwa zimezalishwa nchini, huku  kukiwa na mnyororo wa thamani ambapo uwepo wa wataalamu wa kigeni kupitia vibali 12,549 umesaidia kuzalisha ajira nyingine 242,656 kwa wazawa, hali inayothibitisha kuimarika kwa ushirikishwaji wa Watanzania katika shughuli kubwa za uzalishaji na uhamishaji wa teknolojia.

Vilevile, milango ya ajira nje ya nchi imeendelea kufunguka ambapo Watanzania 6,367 wamefanikiwa kupata nafasi za kazi katika mataifa mbalimbali ikiwemo Saudi Arabia, Qatar, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu, huku Serikali ikiendelea kupanua diplomasia ya ajira katika nchi nyingine zaidi. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Hawa Mchafu, amesisitiza kuwa programu zinazoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu zinalenga kuwajengea vijana misingi imara ya ubunifu itakayowawezesha kujiajiri na kushindana kikamilifu. 

Kamati hiyo imejionea mafanikio ya mafunzo katika fani za uchomeleaji, umeme, mabomba, ushonaji na ufundi wa magari katika vyuo mbalimbali ikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni, huku ikishauri kukamilishwa kwa utoaji wa fedha zilizosalia za uanagenzi ili kuhakikisha malengo ya kuwafikia vijana wengi zaidi yanafikiwa kwa wakati.

mwisho

No comments