SAME WAAMBIWA MNYORORO WA UTALII HAUSTAWI BILA AMANI




MAKAMU wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee John Samuel Malecela, ametoa rai nzito kwa Watanzania akisisitiza kuwa sekta ya utalii na mnyororo wake wa thamani hauwezi kustawi bila kuwapo kwa amani na utulivu wa kudumu nchini.

Mzee Malecela ametoa kauli hiyo wilayani Same mkoani Kilimanjaro wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Utalii la Same Festival, ambapo alibainisha kuwa utalii ni mhimili mkuu wa fedha za kigeni na unategemea zaidi taswira ya usalama ya taifa husika.

Akitoa mfano wa njiwa wanaotimka baada ya kusikia kishindo cha jiwe, Mzee Malecela alisema: “Hata kukiwa na njiwa elfu kumi, jiwe likigonga tu wote wanakimbia. Ndivyo ilivyo kwa watalii; amani ikitikisika, uchumi wa nchi unayumba. Lazima wananchi wang'ang'anie amani ili kuendelea kunufaika na fursa za kiuchumi.”

Aliongeza kuwa misingi ya utalii ni ukarimu, hivyo akawataka wananchi wa Same na Watanzania kwa ujumla kuwa kioo cha mapokezi mema kwa wageni ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo ambayo baadhi ya mataifa duniani yanaitegemea kuendesha serikali zao.

Kwa upande wake, Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Kamishna Emmanuel Sisiya, alisema matamasha hayo yamekuwa chachu ya kuongeza idadi ya watalii. Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha uliopita, wageni 7,700 walitembelea hifadhi hiyo, huku 4,000 miongoni mwao wakiwa ni wazalendo.

Kamishna Sisiya alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji wa mahitaji ya malazi na hoteli ndani ya hifadhi hiyo, akisisitiza kuwa Mkomazi ni sehemu pekee katika Kanda ya Kaskazini ambapo mtalii anaweza kumwona faru mweusi kwa urahisi na ukaribu zaidi.

No comments