MJUMBE MAALUMU WA AU, KIKWETE AREJESHA MATUMAINI SUDAN KUSINI



Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Sham, Rais mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete amekutana na Rais Salva Kiir kujadili utekelezaji wa Mkataba wa Amani wa mwaka 2018 (R-ARCSS).

Katika mazungumzo hayo, Rais Kiir alisisitiza kuwa mchakato wa amani unaendelea, huku serikali ikiendeleza juhudi za majadiliano jumuishi yanayohusisha pande zote, ikiwemo pande ambazo hazijasaini makubaliano hayo.

Lengo kuu, amesema Rais Kiir, ni kufikia mwafaka wa kitaifa kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 2026, ambao utakuwa wa kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 2011.

Lakini ziara ya Kikwete haikuishia tu ndani ya kuta za serikali. Akiwa na dhamira ya kuhakikisha sauti ya kila mmoja inasikika, alikutana na viongozi wa vyama vya upinzani, asasi za kiraia, viongozi wa kidini na wasomi. Dk Kikwete alifanya mashauriano na vyama vya siasa kama SPLM-IG, SPLM-IO na SSOA, pamoja na asasi za kiraia, viongozi wa dini na wanazuoni.

Mkakati huo jumuishi umepongezwa na wadau wengi wa amani, akiwemo mwanaharakati mashuhuri Edmund Yakani, aliyesema kuwa uzoefu wa Kikwete katika upatanishi ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuwaleta watu wote kwenye meza ya mazungumzo, hata wale wenye mitazamo tofauti.

Uzito wa ziara hii unachochewa na historia ya Kikwete nchini humo. Mwaka 2015, yeye ndiye aliyekuwa kiungo muhimu katika kufanikisha Makubaliano ya Arusha yaliyowatunanisha wanachama wa SPLM.

Kabla ya kutua Juba, Kikwete alishafanya mazungumzo na marais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Yoweri Museveni wa Uganda, ambao ni wadhamini wakuu wa amani ya Sudan Kusini. Hatua hizi zinaashiria kuwa Umoja wa Afrika sasa umejipanga dhabiti kuivusha nchi hiyo kutoka kwenye misukosuko na kuingia katika kipindi kipya cha neema na utulivu.

 

No comments