MKAPA KUFUNGWA MIEZI SITA: SERIKALI YAANZA RASMI MABADILIKO MAKUBWA YA PITCH
Serikali imeanza rasmi kazi ya ukarabati mkubwa wa eneo la kuchezea (pitch) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Mradi huu unahusisha uondoshaji wa nyasi za zamani na uwekaji wa nyasi mpya za asili (natural grass) utakaotekelezwa na kampuni ya Reform Sports kutoka nchini Uturuki kwa muda wa takribani miezi sita. Katika kipindi hiki, uwanja utafungwa kwa shughuli zote za michezo ili kuruhusu wataalamu kukamilisha kazi hiyo kwa viwango vya kimataifa vinavyohitajika.
Akizungumzia maboresho hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amebainisha kuwa marekebisho haya yataifanya pitch ya Mkapa kuwa ya kisasa na yenye tija kwa miaka mingi ijayo.
Amewaomba radhi wapenzi wa kandanda nchini kwa kuikosa dabi ya Kariakoo ya tarehe 3 Mei, 2026 katika dimba hilo (Lupaso), akisisitiza kuwa baada ya kazi hiyo kukamilika, uwanja utakuwa katika hali bora wakati wote.
Aidha, amewataka wadau kukaa tayari kwa mabadiliko makubwa yatakayohusisha pia maeneo ya kupumzikia (lounges), vyumba vya kubadilishia nguo (changing rooms), ubao wa matokeo (score board) pamoja na muonekano wa jumla (branding).
Sababu kuu ya uwekezaji huu ni kukidhi vigezo vikali vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na FIFA kuelekea AFCON 2027. Ili uwanja upate kibali cha wenyeji, eneo la kuchezea lazima liwe na ubora wa juu unaohakikisha usalama wa wachezaji na kuruhusu matangazo ya televisheni kuwa na muonekano wa kuvutia duniani kote. Maboresho haya yanalenga kuondoa changamoto zote za kiufundi zilizokuwepo awali na kuimarisha hadhi ya Tanzania katika ramani ya miundombinu bora ya michezo barani Afrika.
Mbali na kukidhi vigezo vya AFCON, uwekaji wa nyasi hizi mpya utaboresha kiwango cha soka kwa kuruhusu mpira kutembea kwa kasi na ufundi, huku ukipunguza hatari ya majeraha kwa wachezaji.
Kazi hii pia inahusisha ukarabati wa mfumo wa mifereji ya maji chini ya ardhi (drainage system) ili kuzuia dimba lisiingie maji wakati wa mvua kubwa, hali inayohakikisha mechi zinaendelea bila usumbufu. Hatua hii itaufanya uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa na hadhi ya kisasa zaidi kwa matumizi ya michezo ya ndani na ile ya kimataifa.
Ushiriki wa kampuni ya Reform Sports unatoa uhakika wa ubora wa mradi huu kutokana na uzoefu wao wa zaidi ya miongo mitatu katika ujenzi wa miundombinu ya michezo katika nchi zaidi ya 100. Kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika uwekaji wa nyasi na mifumo ya umwagiliaji, kampuni hiyo inatarajiwa kuufanya Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa na eneo la kuchezea lenye viwango sawa na viwanja vinavyotumika katika ligi kuu maarufu duniani, jambo litakalokuwa fahari kwa Taifa.
Post a Comment