MSOMI WA UDOM ASHINDA TUZO KUBWA YA FILAMU NCHINI CHINA
Tasnia ya sanaa na utamaduni nchini Tanzania imepata heshima kubwa ya kimataifa baada ya Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Suleiman Risasi, kuibuka mshindi katika Tamasha la Filamu la Kimataifa la Beijing (BJIFF) nchini China.
Risasi amejinyakulia Tuzo ya Makala Fupi Bora kupitia kazi yake ya ubunifu iitwayo ‘The Spirit of the Silk Road’, iliyoshindanishwa katika kipengele cha vijana ndani ya kitengo cha filamu fupi.
Tamasha hilo la 16 la Beijing, ambalo lilihitimishwa rasmi juzi baada ya kudumu kwa siku 10 kuanzia Aprili 15, linatajwa kuwa moja ya majukwaa makubwa na yenye ushawishi zaidi duniani katika ulimwengu wa sinema.
Ushindi wa Risasi umekuja baada ya kazi yake kupita kwenye mchujo mkali ulioshirikisha maelfu ya watayarishaji na wabunifu kutoka mataifa mbalimbali, ikionyesha uwezo mkubwa wa watanzania katika ushindani wa kimataifa.
Jopo la majaji katika tamasha hilo limeisifu kazi ya Risasi kama kielelezo cha juu cha ubunifu kinachotumia teknolojia ya kisasa kusimulia urithi wa kihistoria wa "Njia ya Hariri" (Silk Road).
Makala hiyo imeelezwa kuwa na uwezo wa kipekee wa kuunganisha tamaduni na kuleta uelewa mpya wa mahusiano ya kibinadamu kupitia picha jongefu, jambo lililoifanya iguse hisia za hadhira ya kimataifa na majaji kwa ujumla.
Kufuatia ushindi huo wa kihistoria, Bodi ya Filamu Tanzania imetoa pongezi za dhati kwa mshindi huyo ikisema kuwa mafanikio yake ni fahari kwa Taifa na kielelezo cha kukua kwa vipaji vya ndani. Bodi imesisitiza kuwa ushindi huu unapaswa kuwa chachu kwa wasanii na vijana wengine nchini kuongeza weledi na ubunifu ili kuitangaza Tanzania vizuri zaidi kupitia sanaa ya filamu.
Kwa upande wake, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeelezea ushindi huo kama uthibitisho wa ubora wa taaluma zinazotolewa chuoni hapo, hususani katika Ndaki ya Sayansi za Jamii na Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari. Uongozi wa chuo umesema kuwa mafanikio ya Suleiman Risasi yanaipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimasomo na kisanaa, huku yakithibitisha kuwa wataalamu wa ndani wana uwezo wa kuzalisha kazi zenye viwango vya hali ya juu vinavyokubalika duniani kote.

Post a Comment