MAJERUHI WA VURUGU ZA UCHAGUZI AISHUKURU SERIKALI KUKUBALI PENDEKEZO LA TIBA




Mmoja wa majeruhi wa vurugu zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Idd Omary, ameishukuru Serikali kufuatia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeeleza kuwa Serikali itagharamia matibabu ya majeruhi wote waliotokana na ghasia hizo. 

Rais Samia alitoa kauli hiyo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mapendekezo ya tume, wakati alipokuwa anakabidhiwa taarifa rasmi na Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman kuhusu vurugu hizo zilizotikisa nchi tarehe 29 Oktoba. 

Omary ameeleza kuwa licha ya kuendelea kupata nafuu, bado anakabiliwa na matibabu ya muda mrefu kutokana na vyuma alivyofungiwa mguuni na madaktari, ambapo ameshauriwa kusubiri mguu upone kabla ya kufanyiwa upasuaji mwingine wa kuviondoa, hivyo msaada huo wa serikali utakuwa mkombozi mkubwa kwake.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Mugisha Nkoronko, ameunga mkono uamuzi huo akisema kuwa ni habari njema kwa waathirika, hasa kwa wale ambao wamepata ulemavu wa kudumu ikiwemo kukatwa miguu kabisa na wanahitaji msaada huo wa dharura. 

Dk. Nkoronko amesisitiza kuwa sasa kinachotakiwa ni kuwekwa kwa utaratibu rasmi na wa haraka wa kuwabaini waathirika wote ili waweze kupata huduma hizo stahiki. 

Amebainisha kuwa Tanzania ina vituo vyenye uwezo mkubwa wa kutengeneza viungo bandia na kutoa huduma za kibingwa, ikiwemo Hospitali ya Benjamin Mkapa, KCMC, na Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), hivyo maelezo mahususi yanahitajika kwa wananchi namna ya kufika katika vituo hivyo ili kupata matibabu hayo yaliyoelekezwa na mkuu wa nchi.

Wakati juhudi za tiba ya miili zikiendelea, wataalamu wa saikolojia wameshauri serikali kutoishia kwenye matibabu ya majeraha ya nje pekee, bali kuandaa mpango wa kutumia wataalamu wa afya ya akili kuwasaidia waathirika kurejea katika hali zao za kawaida. 

Imekuwa ikielezwa kuwa wengi wa waliohusika au kuathirika na vurugu hizo bado wana makovu ya kisaikolojia yanayohitaji ushauri wa kitaalamu ili kuimarisha amani na utulivu wa kudumu miongoni mwa wananchi. 

Hatua hii ya Rais Samia kuanza na uponyaji wa wale walioumia zaidi, inatafsiriwa kama dhamira ya dhati ya kuliunganisha taifa na kutekeleza kwa vitendo falsafa ya maridhiano ambayo imekuwa dira ya uongozi wake tangu aingie madarakani.

Ripoti ya Tume ya Jaji Chande ilibainisha kuwa jumla ya watu 518 walipoteza maisha katika vurugu hizo, huku raia zaidi ya 2,390 wakiwa majeruhi.

No comments