VYAMA 12 VYA SIASA VYAPONGEZA RIPOTI YA JAJI CHANDE, VYAHIMIZA KATIBA MPYA NA MARIDHIANO




Umoja wa vyama 12 vya siasa nchini umetoa tamko la kupongeza Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Tarehe 29 Oktoba na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 iliyowasilishwa na Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, ukisema kuwa ni mwongozo sahihi wa kurejesha amani na utulivu wa kudumu nchini. 

Katika mkutano wao  na waandishi wa habari, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ukomavu wa kisiasa alioonesha kwa kukubaliana na mapendekezo yote 12 ya muda mfupi na yale ya muda wa kati yaliyotolewa na Tume hiyo kwa ajili ya kuliponya taifa.

Mheshimiwa Doyo amesisitiza kuwa miongoni mwa mapendekezo hayo, pendekezo la nne na la tano yanapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka na mamlaka husika ili kuondoa mzozo wa kisiasa uliopo nchini na kujenga misingi imara ya kidemokrasia. 

Pendekezo la nne linasisitiza umuhimu wa Tanzania kupata Katiba Mpya ifikapo mwaka 2028 ili itumike katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2029 na uchaguzi mkuu wa 2030, ambapo serikali imetakiwa kuunda Kamati ya Wataalamu wa Katiba itakayopitia nyaraka zote za kihistoria ikiwemo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba na Katiba Pendekezwa ya mwaka 2014 ili kuandaa rasimu itakayopigiwa kura ya maoni na wananchi.

Aidha, wadau hao wamepigia debe pendekezo la tano linaloitaka Serikali kuunda Tume ya Maridhiano na Muafaka wa Kitaifa kupitia mamlaka ya Rais chini ya Ibara ya 36 ya Katiba ya nchi, itakayokuwa shirikishi katika nyanja za kisiasa, kijamii, na kiuchumi. 

Tume hiyo inatajwa kuwa chombo muhimu kitakachosimamia tathmini ya ukweli, kuponya majeraha ya waathirika, na kutafuta suluhisho la kudumu la kisiasa ili kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa ambao umekuwa sifa kuu ya Tanzania duniani kote.

Vyama vilivyotoa msimamo huo wa kizalendo ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), CHAUMMA, CCK, Chama cha MAKINI, UPDP, na NLD, huku vingine vikiwa ni CUF, NRA, TLP, UMD, TADEA, pamoja na AAFP. 

Hatua hii ya vyama vya siasa kuungana na kupongeza ripoti hiyo inatafsiriwa kama ishara ya kurejea kwa ukomavu wa kisiasa nchini, ambapo maslahi ya taifa na amani ya mwananchi wa kawaida yanawekwa mbele ya itikadi za vyama. 

Watanzania wameendelea kuonyesha kuwa wanaitaka amani kwa gharama yoyote, na utekelezaji wa mapendekezo hayo ya Tume ya Jaji Chande unatajwa kuwa ndio mwarobaini utakaohakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa kisiwa cha amani na utulivu.


No comments