DKT. MWIGULU: TUNAFUATILIA KWA UMAKINI SUALA LA MAFUTA



 

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuendelea kuwa watulivu na kwamba Serikali inafuatilia kwa karibu na kwa umakini suala la mafuta na kuhakikisha yanaendelea kupatikana nchini ili shughuli za uzalishaji na usafirishaji zisiathirike.

 

Amesema kuwa suala la upatikanaji wa mafuta si jambo la kuamliwa na nchi moja kwa sababu si kila nchi ni muagizaji au mzalishaji wa bidhaa hiyo.”Niwahakikishie Serikali inafuatilia na kila siku kuna vikao tunakaa vya sekta mbalimbali kuweza kuhakikisha  kwamba bidhaa hii haiadimiki na tunashughulika na masuala ya bei ya bidhaa na bei ya huduma.”

 

Waziri Mkuu amesema kwa kutambua umuhimu wa bidhaa hiyo Serikali imelenga kuendelea kuhakikisha inalinda maslahi mapana ya Watanzania kwa sababu haitaki watu washindwe kumudu kupata bidhaa wala kuendesha maisha.

 

Ameyasema hayo Jumapili, Aprili 12, 2026 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mvumi Mision akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Chamwino, Dodoma.

 

Amesema ni kweli suala hilo litasababisha madhara si kwa Tanzania tu bali hata kwa nchi inapopiganiwa vita na pamoja na nchi ambazo hazipo kwenye vita kwa sababu mnyororo huo wa usambazaji wa bidhaa unaathirika na hicho kinachoendelea.

 

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuzungumza na watoa huduma ili kufanya tathmini ya kina na kuchukua hatua bila ya kuleta taharuki, hivyo amewasisitiza Watanzania kuendelea kuwa watulivu.

 

Amesema suala kama hilo liliwahi kutokea nchini na kwamba miongozo na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliliwezesha Taifa kuvuka salama na hata sasa hatua zinachukuliwa kuhakikisha suala la mafuta haliathiri ukuaji wa uchumi.

 

No comments