Dakika Sita za Mashaka ya Mwanadamu , Orion ikikata angahewa kurejea duniani



Dakika sita za ukimia wa ukiwa wenye kutisha zilianza pale chombo cha Orion kilipogusa angahewa ya Dunia kwa kasi ya kilometa 40,000 kwa saa huku kikiwa kimezungukwa na utando wa plasma uliokata mawasiliano yote kati ya wanaanga na dunia. 

Katika chumba cha udhibiti cha NASA jijini Houston hali ya wasiwasi ilitanda huku wataalamu wakitazama skrini ambazo hazikuwa na ishara yoyote wakijua fika kuwa ngao ya joto ya chombo hicho ndiyo ilikuwa kizuizi pekee kati ya maisha ya mashujaa wanne na joto kali la nyuzi maelfu linaloweza kuyeyusha chuma. 

Mkurugenzi wa safari, Rick Henflig alikiri baadae kuwa yeyote ambaye hangehisi mapigo ya moyo kwenda mbio katika muda huo basi hakuwa na uhai kwani sekunde zilijivuta kama saa huku kila mmoja akisubiri kusikia sauti ikirejea kutoka kwenye giza la mawasiliano baada ya safari ya siku kumi kuzunguka Mwezi.

Mwanaanga  Victor Glover, ambaye ni rubani wa Artemis II (kushoto), na Christina Koch, mtaalamu wa misheni ya Artemis II, wakiwa wameketi kwenye helikopta ya Jeshi la Majini ya Marekani aina ya MH-60 Seahawk ya Kikosi cha 23 cha Helicopter Sea Combat (HSC) katika manowari ya   USS John P. Murtha.Picha hii imechnukuliwa baada ya wao na wenzao,  Jeremy Hansen, mtaalamu wa misheni ya Artemis II,  Reid Wiseman, kamanda wa Artemis II, kutolewa kwenye chombo chao cha Orion baada ya kutua salama majini (splashdown) Ijumaa, Aprili 10, 2026, katika Bahari ya Pasifiki pwani ya California.


Ghafla ukimya huo ulivunjika kwa sauti ya kishindo cha redio ikifuatiwa na taswira ya miamvuli mikuu iliyofunguka vizuri angani na kuanza kukishusha chombo hicho taratibu kuelekea kwenye maji tulivu ya Bahari ya Pasifiki mnamo Aprili 10, 2026. Orion ilifanikiwa kuvuka salama kizuizi tishio la kurejea duniani,mpaka wa angahewa.

Shangilio kubwa lililipuka ndani ya Mission Control na kwenye meli ya uokoaji ya USS John P. Murtha pale Orion ilipofanya splashdown ( kutua salama baharini ) saa mbili na dakika saba usiku huku ikithibitisha kuwa binadamu amerejea rasmi kwenye ulingo wa anga za mbali baada ya miaka hamsini na tatu tangu safari za Apollo zilipokoma. 

Mwanaanga Edwin E. Aldrin Jr., rubani wa chombo cha kutua mwezini (LM) katika misheni ya kwanza ya kutua kwenye mwezi, akiwa amesimama kando ya bendera ya Marekani iliyopandwa kwenye uso wa mwezi. Chombo cha Eagle kinaonekana upande wa kushoto, huku nyayo za miguu ya wanaanga zikionekana wazi kwenye udongo wa mwezi. Picha hii ilipigwa na Kamanda Neil A. Armstrong kwa kutumia kamera ya 70mm Hasselblad. Wakati Armstrong na Aldrin wakifanya utafiti katika eneo la Sea of Tranquility, mwanaanga Michael Collins alibaki kwenye mzunguko wa mwezi akiongoza chombo cha Columbia.Tarehe ya Tukio: 1969-07-21


Hatua hiyo ya kugusa maji haikuwa tu mwisho wa safari ya kilometa mamilioni bali ilikuwa ni uthibitisho wa teknolojia ya kisasa na ujasiri wa binadamu uliovuka mipaka kama alivyosema meneja wa mradi, Howard Hu.

Mafanikio ya Artemis 2 yana maana kubwa kwa shirika la NASA na binadamu kwa ujumla kwani yamefungua mlango ambao ulikuwa umefungwa kwa miongo mingi kuelekea kwenye uso wa Mwezi na hatimaye sayari ya Mars. 

Msimamizi wa NASA, Jared Isaacman alishindwa kuzuia hisia zake akieleza kuwa huu ni wakati ambao ulimwengu uliusubiri kwa maisha yote akiamini kuwa sasa hatuendi tena Mwezini kupanda bendera na kuondoka bali tunakwenda kuishi na kujenga makazi ya kudumu. 




Kufanikiwa kwa safari hii kumeweka msingi imara kwa mradi wa Artemis 3 utakaoshuhudia binadamu akikanyaga tena ardhi ya Mwezi huku kukiwa na matumaini makubwa ya kuanza kwa ujenzi wa vituo vya utafiti vitakavyosaidia kuelewa asili ya mfumo wetu wa jua.

Kurudi kwa Orion kumeandika ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimataifa na uvumbuzi ambapo kila tone la jasho la maelfu ya wataalamu waliofanya kazi usiku na mchana sasa limezaa matunda ya kishindo. Dunia nzima sasa inatazama mbele kwa shauku ikijua kuwa njia kuelekea juu imesafishwa na kazi iliyo mbele yetu ni kubwa zaidi kuliko ile iliyopita kwani safari ya sasa ni ya kudumu na yenye malengo mapana zaidi ya kisayansi. Huu ni ushindi wa moyo wa binadamu usiochoka kutafuta maarifa na ni zawadi kwa vizazi vijavyo vitakavyoona Mwezi si kama kitu cha mbali kinachong'aa angani bali kama kituo kingine cha nyumbani kwa mwanadamu.



No comments