CHAKWERA APIGILIA MSUMARI JITIHADA ZA MARIDHIANO



JUMUIYA ya Madola imeipa Tanzania heshima kubwa na kuunga mkono kwa dhati mchakato wa kutafuta suluhu ya kudumu kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoibuka wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Msimamo huo mzito umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais Mstaafu wa Malawi, Dk. Lazarus Chakwera, ambaye yuko nchini kama Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola. Dk. Chakwera amewasha taa ya kijani kwa kuridhishwa na ukomavu ambao Tanzania inauonyesha katika kuikabili changamoto hiyo kupitia njia ya mazungumzo na maridhiano.

Saa Mbili za Kimkakati Ndani ya BoT

Katika kikao cha siri na kizito kilichodumu kwa takribani saa mbili ndani ya Jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ujumbe huo wa Madola ulipata wasaa wa kupigwa msasa na Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani.

Dk. Chakwera, akizungumza kwa mamlaka na upendo kwa Tanzania, alisisitiza kuwa Jumuiya ya Madola haiko hapa kutazama tu, bali kusaidia juhudi za kurejesha amani kamili. "Naipenda Tanzania na nimefurahishwa na kinachoendelea. Kila upande unatafuta suluhu na hicho ndicho tunachokitaka. Jumuiya ya Madola iko bega kwa bega na Tanzania," alisema kiongozi huyo.

Jaji Chande Afunguka: Hadidu za Rejea Ziko Wazi

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, ameweka mambo hadharani kuwa mazungumzo hayo yamekuwa ya uwazi na tija. Jaji Chande alibainisha kuwa walitumia muda huo kuelezea kwa kina majukumu ya tume na namna hadidu za rejea zinavyotekelezwa kwa ufanisi bila upendeleo.

"Tumeeleza majukumu ya tume na hadidu za rejea ambazo ziko wazi, pamoja na namna kazi yetu inavyokwenda. Tumejibu maswali yote ya ufafanuzi kwa ufasaha," alieleza Jaji Chande, akionyesha utayari wa tume yake kukamilisha jukumu hilo nyeti kwa maslahi mapana ya Taifa.

Diplomasia ya Amani: Tanzania Kwenye Ramani

Ujio wa Dk. Chakwera unatafsiriwa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa kama hatua kubwa ya kidiplomasia kwa Tanzania. Hatua ya serikali kuunda tume hiyo na kuikaribisha Jumuiya ya Madola inaashiria nia ya dhati ya kuimarisha utawala wa sheria na kulinda sifa ya nchi kama kisiwa cha amani barani Afrika.

Kazi ya tume hiyo sasa inaingia kwenye hatua muhimu, huku macho ya Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa yakiwa yameelekezwa Dar es Salaam kusubiri matokeo ya uchunguzi huo yatakayoweka msingi mpya wa umoja na utulivu wa kitaifa.

No comments