ASHAURI UTII KWA VYAMA VYA SIASA USIZIDI UTAMBULISHO WA KITAIFA
Mustakabali wa Tanzania unategemea uwezo wa viongozi na wananchi wake kukumbatia mazungumzo, kuheshimu tofauti na kuliweka taifa mbele ya maslahi binafsi ili kulinda tunu ya amani iliyodumu kwa miongo kadhaa.
Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Almas, anasisitiza kuwa umoja wa kitaifa si jambo la bahati mbaya, bali ni matokeo ya juhudi za makusudi za viongozi na wananchi kuweka mbele maslahi ya pamoja kuliko itikadi za vyama. Akizungumzia hali ya sasa, Almas anaonya kuwa ikiwa utii kwa vyama vya siasa utazidi utambulisho wa kitaifa, itakuwa vigumu kudumisha mshikamano ambao ndio injini kuu ya maendeleo, huku akibainisha kuwa bila umoja nchi inaweza kukumbwa na changamoto za kupungua kwa imani ya wawekezaji na machafuko ya kijamii.
Katika kuelezea umuhimu wa taasisi imara, Almas anasema anatambua nafasi ya vyama vya siasa katika kujenga utawala bora na kutoa mawazo mbadala, lakini anasisitiza kuwa shughuli zote zinapaswa kufanyika ndani ya mfumo unaolinda umoja wa taifa.
Katika mazunbgumzo hayo alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mfumo wake wa uongozi unaozingatia ushirikishwaji na mazungumzo, akiamini kuwa falsafa ya R 4 ambayo inajumuisha Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya ndiyo nguzo muhimu ya kuimarisha umoja huo. Kwake yeye, maridhiano ni hatua muhimu ya kuponya majeraha ya kisiasa na kuhakikisha kuwa nchi inasonga mbele kwa amani licha ya tofauti za kimitazamo.
Akirejelea vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, Almas anasema matukio hayo yalionesha hatari ya kuporomoka kwa mshikamano wa kitaifa na umuhimu wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Anaeleza imani yake kubwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani inayowasilisha taarifa yake, akitarajia kuwa itatoa majibu yenye haki na uwiano yatakayosaidia kuimarisha utamaduni wa kuheshimiana.
Anatoa onyo kali dhidi ya matumizi ya lugha za chuki na migongano ya kisiasa akisema kuwa mambo hayo yanadhoofisha mazungumzo ya kujenga na kuhatarisha usalama wa muda mrefu wa taifa.
Almas anasisitiza kuwa kila mwananchi ana jukumu la kulinda amani na kuheshimu utawala wa sheria kama njia pekee ya kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi yenye amani na mshikamano. Kwake, uimara wa taifa upo katika uwezo wa wananchi wake kubaki wamoja na kuheshimiana, huku wakijua kuwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii hayawezi kupatikana katika mazingira ya vurugu na kutokuaminiana.
Post a Comment