KONYAGI YAZINDUA KIZIBO KIPYA CHA KIDIGITALI KUIMARISHA USALAMA WA WANYWAJI



Kinywaji maarufu nchini cha Konyagi, kinachofahamika kama "Roho ya Taifa" (Spirit of the Nation), kimetangaza mabadiliko makubwa ya muonekano wa kizibo chake ikiwa ni hatua ya kuimarisha usalama na kulinda ubora wa kinywaji hicho dhidi ya bidhaa feki.

Mabadiliko hayo yanahusisha chupa za mililita 200, 500, na 750, ambapo sasa kizibo hicho kimeongezewa teknolojia ya picha inayocheza (hologram). Mtumiaji anapoinamisha chupa mbele na nyuma, herufi "K" kwenye kizibo hugeuka na kuonekana picha ya "Shujaa wa Kizaramo," alama ambayo imekuwa utambulisho wa Konyagi tangu ilipoanzishwa Kariakoo mwaka 1970.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Michelle Kilpin, amesema kuwa kizibo hicho kipya kimeundwa kutoa sauti ya kipekee ya kukatika wakati wa kufunguliwa, huku chupa ya mililita 750 ikiongezewa mstari wa dhahabu (gold band) unaoonekana mara baada ya kufunguliwa kwa mara ya kwanza. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa mtumiaji ana uhakika na kile anachokunywa kabla hata hajaonja.

Licha ya mabadiliko hayo ya kiteknolojia, taarifa hiyo imesisitiza kuendelea kuenzi mila na utamaduni wa Watanzania unapoifurahia Konyagi. Hii ni pamoja na utamaduni wa "kuipa heshima yake" kwa kuilaza chupa katikati ya meza baada ya kuwamiminia wenzao, ishara inayotafsiriwa kama usawa na upendo miongoni mwa marafiki.

No comments