Miaka 64 ya Uhuru Tanzania Bloggers Network yasisitiza utulivu na amani
Leo Desemba 9, tunapoadhimisha miaka 64 tangu Taifa letu lipate Uhuru, TBN (Tanzania Bloggers Network) inatoa pongezi za dhati kwa kila Mtanzania. Siku hii si tu ya mapumziko, bali ni fursa muhimu ya kutafakari safari tuliyotoka, mahali tulipo, na tunapoelekea kama Taifa moja.
Waasisi wetu walitupatia Uhuru ili tuweze kujitegemea na kujenga nchi yetu wenyewe. Leo, kupitia mitandao yetu, tunawakumbusha Watanzania kauli thabiti ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliposema:
"Uhuru hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea. Hatuwezi kuitwa huru kama tunategemea wengine kutupatia mahitaji yetu ya kimsingi."
Jukumu letu: Tujenge Taifa, Tuache Kulibomoa
Kama chombo cha habari za kidijitali na mitandao, TBN inasisitiza kuwa mafanikio yote tuliyonayo yametokana na utulivu na mshikamano. Ili kuendeleza gurudumu la maendeleo, kama waasisi wetu walivyofanya, tunahitaji utulivu, amani na maridhiano. Kinyume na hapo, hatuwezi kujenga.
Tunawakumbusha Watanzania umuhimu wa amani kama msingi wa kila kitu, kama alivyowahi kusema Rais mstaafu Benjamin William Mkapa:
"Amani si kitu cha asili, tunahitaji kuilinda na kuitunza kila siku. Bila amani, hakuna maendeleo ya kweli."
Tukiruhusu vurugu na uchochezi, juhudi zote za waasisi wa taifa hili za kupambana na maadui wakuu watatu—ujinga, umaskini na maradhi—zitadhoofishwa zaidi. Tunapaswa kuacha kuwa chombo cha kuharibu Taifa letu.
Kuheshimu Zama na Mwelekeo wa Uongozi
Kila kizazi na utawala una jukumu la kuendeleza gurudumu la Taifa. Tunakumbuka kauli ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyewahi kusema:
"Kila utawala na zama zake. Kila kiongozi na mchango wake katika ujenzi wa Taifa hili."
Kwa sasa, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Taifa letu linajikita katika msingi wa 4R (Reconciliation, Resilience, Reforms, and Rebuilding). Tunawasisitiza Watanzania wote kuunga mkono juhudi hizi za maridhiano na mageuzi zinazolenga kuleta ustawi wa pamoja.
Watanzania, tunayo nafasi ya kuzungumza, tuzungumze. Tusiitumie nafasi hiyo kubomoa Taifa bali kulijenga. Ni wajibu wetu kuthamini uhuru huu kwa kufanya kazi kwa bidii, kudumisha amani, na kuacha kutumika kama chombo cha kuharibu nchi.
TBN inawatakia Maadhimisho Mema ya Miaka 64 ya Uhuru!
Tanzania Kwanza,Kazi na Utu Tusonge Mbele
Beda Msimbe
Mwenyekiti TBN

Post a Comment