WAAMUZI, KLABU, WACHEZAJI DABI YA KARIAKOO WAKIONA CHA MOTO



Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imechukua hatua kali dhidi ya waamuzi na wachezaji kufuatia mfululizo wa makosa ya kiufundi na utovu wa nidhamu. 

Hatua hizo zimekuja baada ya mchezo wa dabi ya Kariakoo kati ya Yanga na Simba uliopigwa Machi Mosi, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kule Unguja, kumalizika kwa suluhu huku kukiwa na malalamiko ya uamuzi.

Katika rungu hilo la adhabu, mwamuzi msaidizi namba moja, Kassim Mpanga, amefungiwa miezi sita kwa kukataa bao halali la Simba dakika ya 70 kwa kisingizio cha kuotea, uamuzi ambao tathmini ya wataalamu imebaini ulikuwa wa makosa. 

Vivyo hivyo, mwamuzi msaidizi namba mbili, Hamdan Said, amefungiwa miezi mitatu baada ya kusimamisha shambulizi la Yanga dakika ya 61 akidai mchezaji Prince Dube alikuwa ameotea, jambo ambalo pia lilithibitika kuwa si kweli kulingana na sheria za soka.

Mbali na dabi hiyo, waamuzi wengine waliokumbwa na rungu ni Abdallah Mwinyimkuu aliyeshushwa daraja kwa makosa ya kujirudia kwenye mchezo wa Yanga na Namungo, pamoja na Charles Simon aliyefungiwa miezi mitatu kwa kuruhusu Dodoma Jiji kufanya mabadiliko ya wachezaji mara nne badala ya tatu katika mchezo wao dhidi ya Simba. Adhabu hizi zinalenga kuimarisha viwango vya uamuzi na haki uwanjani katika michezo inayofuata ya Ligi Kuu.

Kwa upande wa wachezaji, Selemani Mwalimu wa Simba na Abdi Banda wa Dodoma Jiji wamefungiwa michezo mitatu na kupigwa faini ya Shilingi milioni moja kila mmoja kwa makosa ya kumpiga mpinzani kiwiko na mchezo wa kuigiza wa kupoteza muda mtawalia. 

Aidha, wachezaji wengine kama David Kameta wa Simba wametozwa faini kwa makosa ya kishirikina, huku vilabu vya Yanga na Simba vikitozwa faini nzito za Shilingi milioni 5 na milioni 20 kwa makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu na ukiukwaji wa kanuni za ligi.


No comments