Kutoka Kanisani Hadi Shambani: Simulizi ya Sista Aliyenolewa na Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi
Na Mwandishi Wetu, Laela Rukwa
Katika kuta za utulivu za Chuo cha Kilimo na Mifugo cha Kanisa Katoliki kilichopo Laela, mkoani Rukwa, sauti ya shukrani imesikika kutoka kwa mtawa mmoja aliyepata fursa ya kipekee ya kujinoa kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi (Uanagenzi).
Mtawa huyo, Sista Vestina Damian ambaye sasa amekuwa ishara ya matumaini na weledi, anasimulia jinsi mafunzo ya vitendo aliyoyapata yalivyomgeuza kutoka kuwa mwanafunzi wa nadharia na kuwa mtaalamu aliyepikwa vyema.
Maelezo hayo yalitolewa mbele ya Maofisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano wakiongozwa na Msemaji Mkuu wa Ofisi hiyo Revocatus Kassimba waliofika chuoni hapo kufuatilia utekelezaji wa mafunzo ya uanagenzi.
Sista Vestina Damian, akiwa mmoja wa wanufaika wa programu hiyo, alieleza kwa msisitizo namna mafunzo hayo ya uanagenzi yaliyochukua miezi minane yalivyomjengea weledi wa kitaalamu katika kilimo na ufugaji wa kisasa.
Alibainisha kuwa, kupitia mchanganyiko wa nadharia na vitendo, ameweza kujifunza mbinu za kisasa za kilimo cha umwagiliaji, matumizi sahihi ya mbolea, na mbegu bora zinazohimili mabadiliko ya tabianchi, maarifa ambayo sasa anayatumia kuifanya bustani na mashamba ya utawani kuwa mfano wa kuigwa katika eneo la Laela.
Upande wa mifugo, Sista huyo alieleza kuwa programu hiyo imemsaidia kuelewa kanuni za kitaalamu za ufugaji wa kisasa, ikiwemo ujenzi wa maboma bora, utayarishaji wa lishe mchanganyiko, na udhibiti wa magonjwa.
Alibainisha kuwa maarifa hayo aliyopata yamemwezesha kusaidia jamii inayomzunguka na hivyo kukuza tija katika kilimo na ufugaji, jambo ambalo linaendana na dhamira ya Serikali ya kuongeza tija na uzalishaji ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi.
“Ujuzi huu umenipa heshima kubwa kwa jamii yanguj kwani umenipa uwezo wa kuhudumia watu wangu kwa weledi zaidi,” alieleza Sista Vestina Damian mbele ya maofisa hao na wanajamii wengine.
Akiwa amevalia mavazi yake ya kitawa , Sista Vestina Damian anasifu uamuzi wa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) kwa kuweka mfumo unaoruhusu wananchi wa kada zote kupata ujuzi stahiki. Kwake, uanagenzi huo haukuwa tu mafunzo ya darasani, bali ulikuwa ni ukombozi wa fikra uliompa ujasiri wa kwenda kusimamia miradi ya uzalishaji inayolenga kuwasaidia wahitaji na jamii inayomzunguka.
"Naishukuru Serikali, namshukuru mama Samia kwa kutupa fursa hii sisi wananchi wake, bila kujali nafasi zetu," anasema Sista Vestina Damian huyo kwa unyenyekevu.
Alisisitiza katika shukurani zake kuwa ujuzi alioupata chuoni Laela ni hazina itakayotumika kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla, huku akitoa rai kwa Serikali kuendelea kutanua wigo wa programu hiyo ili kuwafikia vijana na wahitaji wengi zaidi katika maeneo ya pembezoni.
Chini ya kaulimbiu isemayo “Nguvukazi yenye Ujuzi Stahiki kwa Ajira Endelevu,” Serikali imeweka bayana dhamira yake ya kupunguza pengo la ujuzi linalowakabili vijana wengi nchini. Programu hii inalenga kuleta mabadiliko ya kifikra na kiuchumi kwa kutoa mafunzo yanayoakisi mahitaji halisi ya soko la ajira, yakijikita katika mchanganyiko wa nadharia na vitendo.
Uzinduzi wa awamu ya nane ya programu hii, umefanyika Machi 8 mwaka huu.Uendelevu wa programu unakuja wakati ambapo nchi inajipanga kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ikihitaji nguvukazi yenye ushindani wa kimataifa. Katika awamu hii, Serikali imewekeza rasilimali nyingi kuwafikia vijana 5,746 nchi nzima.
Mafunzo yanatolewa kupitia vyuo 46 vilivyosambaa katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, ambapo vyuo 29 ni vya Serikali na 17 ni vya sekta binafsi (ikiwemo Chuo cha Laela).
Programu hii ya uanagenzi ni sehemu ya mikakati ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano katika kuhakikisha kuwa nguvukazi ya Taifa inapata stadi muhimu za kuajirika au kujiajiri, hivyo kuchochea ukuaji jumuishi wa uchumi kuelekea mwaka 2050.
@@@@@@@@@@@@@
Post a Comment