UTULIVU WA MKUNA NAZI WA ZANZIBAR SOMO KWA VIJANA
KATIKA viunga vya Soko la Kibanda Maiti, kishindo cha mashine inayozunguka kwa kasi sasa kimekuwa wimbo wa matumaini kwa Ramtula Makame. Baada ya miaka saba ya kupambana sokoni hapo akiuza nazi kwa njia ya kawaida, mjasiriamali huyu amevunja mnyororo wa mazoea na sasa amepiga hatua kubwa, si tu kwa kuuza nazi, bali kwa kutoa huduma ya kukuna nazi kwa kutumia teknolojia ya mashine inayomwezesha kuhudumia hadi nazi 200 kwa siku.
Siri ya ukuaji wa Ramtula haipo kwenye nguvu za mikono pekee, bali katika uwezo wake wa kupanga mipango ya muda mrefu na kuthubutu kubadili mwelekeo wa biashara yake.
Kwa kipindi cha miezi mitatu sasa tangu aanze kutumia mashine hiyo, ameshuhudia mapinduzi makubwa ya kipato yanayomwezesha kukidhi mahitaji ya familia yake na kujiwekea akiba. Hali hii inathibitisha kuwa mabadiliko ya kimaendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja yanategemea sana uthubutu wa kuwekeza kwenye vitendea kazi vya kisasa vinavyoongeza tija na ufanisi.
Hata hivyo, mafanikio haya ya Ramtula hayakuja kwa bahati mbaya, bali yamebebwa na mazingira tulivu ya nchi. Utulivu na amani iliyopo ndiyo injini inayompa mjasiriamali huyu nafasi ya kuwaza maendeleo, kuweka akiba, na hatimaye kununua vifaa zaidi bila hofu. Amani inampa mkuna nazi huyu utulivu wa akili wa kushindana sokoni, ikimfanya awe kitovu cha huduma inayopendwa na jamii ambayo imepokea uvumbuzi wake kwa mikono miwili.
Simulizi ya Ramtula ni kielelezo tosha kuwa amani inapostawi, mwananchi anapata fursa ya kutengeneza mifumo ya kujiingizia kipato endelevu.
Kupitia nidhamu ya fedha na malengo ya miaka saba, ameweza kugeuza biashara ya kawaida kuwa ya kisasa, akionyesha kuwa umaskini si hatari, bali ni hatua inayoweza kuvukwa kwa mipango madhubuti na utulivu wa kijamii unaoruhusu biashara kuchanua usiku na mchana.
Mkuna nazi huyu amewahimiza vijana kutochagua kazi kwani katika miaka yote aliyofanya kazi , kazi ya kukuna nazi kwa sasa ndio inayomlipa

Post a Comment