RAIS SAMIA APOKEA UJUMBE MAALUM KUTOKA KWA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 11 Machi, 2026, amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres, uliowasilishwa na Mjumbe wake Maalum, Bw. Parfait Onanga-Anyanga, Ikulu Chamwino.
Bw. Onanga-Anyanga yupo nchini kwa ajili ya kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali na kutathmini hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na utawala wa sheria kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025.
Katika mazungumzo hayo, Mjumbe huyo Maalum ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa unatambua na kupongeza hatua za Serikali ya Tanzania baada ya uchaguzi huo, hususan uamuzi wa kuunda Tume Huru ya Uchunguzi, dhamira ya kufanya mazungumzo jumuishi ya kitaifa, pamoja na kuendeleza mchakato wa mabadiliko ya kikatiba.
Amesema kuwa UN inaendelea kuitambua Tanzania kama nchi yenye historia ndefu ya amani na mshikamano, huku akithamini mchango wa nchi katika juhudi za kulinda amani barani Afrika.
Bw. Onanga-Anyanga amemueleza Rais Samia kuwa, katika ziara yake amekutana na kuzungumza na taasisi mbalimbali nchini ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje, Mahakama, Bunge, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, viongozi wa vyama vya siasa, pamoja na Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchunguzi.
Amesisitiza kuwa mashauriano hayo yatauwezesha Umoja wa Mataifa kupata taswira halisi ya uhalisia wa matukio ya Oktoba 2025 na juhudi za Serikali katika utatuzi wa changamoto, jambo litakalosaidia kuimarisha maridhiano na kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za kidemokrasia.
Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshukuru na kupongeza hatua ya Katibu Mkuu wa UN kutuma ujumbe huo ili kusikiliza maoni ya wadau. Amesema Serikali imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio hayo unazingatia misingi ya utawala wa sheria, uwajibikaji na haki.
Rais ameweka wazi kuwa Serikali iko tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayowasilishwa na Tume ya Uchunguzi mara baada ya kukamilika kwa kazi yake, akibainisha kuwa mapendekezo hayo yatakuwa sehemu muhimu ya kuimarisha maridhiano ya kitaifa na mchakato wa marekebisho ya Katiba.
Aidha, amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kukuza demokrasia na utawala bora nchini.
.jpeg)
Post a Comment