RIDHWANI KIKWETE: TUMIENI MFUNGO KULIOMBEA TAIFA AMANI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhwani Kikwete, amewataka wadau wa sekta ya bima na Watanzania kwa ujumla kutumia kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuliombea Taifa amani ili kuchochea kasi ya uwekezaji nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya kufuturisha wadau wa bima iliyoandaliwa na Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), Waziri Kikwete alisema kuwa amani ndiyo msingi mkuu unaoifanya Tanzania kuwa kitovu bora cha uwekezaji, na hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuitunza kupitia fursa za kiroho kama mfungo.
Alibainisha kuwa sekta ya bima ina mchango mkubwa katika kulinda uchumi wa kisasa, kwani inatoa uhakika wa usalama kwa wafanyabiashara na wawekezaji dhidi ya majanga mbalimbali.
Alisisitiza kuwa bila mfumo imara wa bima, ni vigumu kwa Taifa kupata ustawi endelevu wa kiuchumi unaohitajika na serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango (SMZ), Rajab Uweje, alieleza kuwa Shirika la ZIC limekuwa likitekeleza wajibu wake kama kiungo muhimu cha mfumo wa kifedha nchini. Aliongeza kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na wadau kubuni huduma rafiki zitakazowafikia wananchi wengi zaidi na kusaidia kukuza uchumi wa pande zote mbili za Muungano.

Post a Comment