FIFA KUANZA UTARATIBU WA MAPUMZIKO YA MAJI YA DAKIKA 3 KILA KIPINDI
ZURICH, Uswisi
Shirikisho la Kimataifa la Kandanda (FIFA) limetangaza leo kwamba litaanza kutumia utaratibu wa "mapumziko ya kunywa maji" kwa wachezaji wakati wa Kombe la Dunia la Amerika Kaskazini-Kati litakalofanyika mwaka ujao wa 2026.
Utaratibu huu utawapa wachezaji dakika tatu (3) za kunywa maji katika kila kipindi cha mchezo. Jambo hili litatumika katika mechi zote bila kujali hali ya hewa, joto, uwanja, au kama uwanja una paa au la.
Kwa mujibu wa FIFA, mwamuzi atasimamisha mchezo na kutoa mapumziko hayo mara tu dakika 22 zitakapopita katika kila kipindi. Ikiwa mchezo utasimama mapema kidogo—kwa dakika 1 hadi 2—kutokana na majeraha au sababu zingine, mwamuzi anaweza kutumia busara yake kuanzisha mapumziko hayo ya kunywa maji.
FIFA imesema, " Utaratibu huo ni jaribio la kutoa kipaumbele kwa ustawi wa wachezaji na kuhakikisha wanakuwa katika hali bora zaidi."
Uamuzi huu unajibu wasiwasi unaoongezeka kwamba joto kali wakati wa Kombe la Dunia la mwaka ujao linaweza kuhatarisha usalama wa wachezaji. Joto katika Amerika Kaskazini wakati wa miezi ya kiangazi linatarajiwa kuzidi nyuzi joto 35°C, huku kukiwa na maonyo kwamba zaidi ya viwanja 10 kati ya 16 vitakavyotumika katika Kombe la Dunia vitakabiliwa na hali ya "dhiki kali ya joto."
Vyama vya kimataifa vya wanasoka, ikiwemo FIFPro, viliihimiza mara kwa mara FIFA kuchukua hatua zinazohakikisha usalama wa wachezaji. FIFA hapo awali ilianzisha "mapumziko ya kunywa maji" (ambayo pia yaliitwa "mapumziko ya kujipoza") wakati wa Kombe la Dunia la Klabu lililofanyika nchini Marekani kiangazi kilichopita.
Post a Comment