AFCON 2027: ULINZI NI CHUMA, AMANI YETU NDIO FURSA KWA VIJANA!
WAKATI hamu ya michuano ya AFCON 2027 ikizidi kupanda, Serikali imetuma ujumbe mzito: "Tanzania ni salama na ulinzi ni chuma!"
Katika kikao kizito kilichofanyika Dar es Salaam Machi 4, Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi imekutana na Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Michezo kutoka Umoja wa Mataifa (UN), Valerio de Divitiis, kupigilia msumari mkakati wa kuhakikisha kila mgeni na mwenyeji anakuwa salama kama yuko nyumbani kwake.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Boniface Tamba, ameweka wazi kuwa usalama si suala la polisi pekee, bali ni mazingira tulivu yatakayowawezesha vijana na wafanyabiashara kuchangamkia fursa bila hofu.
Tamba alisisitiza kuwa mifumo ya kudhibiti umati na usimamizi wa viwanja itakuwa ya viwango vya dunia, jambo linaloashiria kuwa Tanzania iko tayari kuishangaza Afrika kwa ukarimu na utulivu wa kipekee.
Kwa upande wake, Leodegar Tenga, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, amepigilia msumari kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha AFCON 2027 inavunja rekodi.
Alibainisha kuwa mashindano haya hayataishia kwenye ufundi wa uwanjani pekee, bali yataacha alama ya usalama wa hali ya juu, jambo ambalo ni msingi wa kuvutia wawekezaji na watalii wanaotafuta maeneo yenye amani ya kudumu.
Huu ni ujumbe tosha kwa vijana wanaopoteza muda kusononeka: Usalama huu unaoandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na UN ni "uwanja mweupe" kwenu. Badala ya kuendekeza chuki mitandaoni, ni wakati wa kuthamini utulivu huu na kujiandaa kuvuna "mapesa" ya mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Post a Comment