Tuesday, October 1, 2024
Simba Queens, Yanga Princess hapatoshi
Samatta kundini tena Stars
Saturday, August 10, 2024
Simba kuanza ligi nyumbani, Yanga Ugenini
Simba |
Yanga |
SIMBA na Yanga zinatarajiwa kukutana Oktoba 19, mwaka
huu katika mzunguko wa nane wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika mchezo huo ambao ratiba ilitolewa jana, Simba
itakuwa mwenyeji ikitumia Uwanja wa KMC, Dar es Salaam na itakutana na Yanga
ikiwa na kumbukumbu ya kipigo mara tatu mfululizo, michezo miwili ya Ligi Kuu
msimu uliopita na juzi kwenye Ngao ya Jamii.
Aidha, Simba inatarajiwa kuanzia kurusha karata yake
ya kwanza ikicheza na Tabora United, Agosti 18 Uwanja wa KMC, Mwenge Dar es
Salaam.
Bingwa mtetezi Yanga wataanza kusaka ubingwa wa nne
mfufulizo ikicheza na Kagera Sugar ugenini Agosti 29 katika Uwanja wa Kaitaba,
Bukoba.
Agosti 16, mwaka huu, wageni kwenye ligi hiyo Pamba
Jiji watawakaribisha Tanzania Prisons katika Uwanja wa Kirumba, Mwanza, Agosti
17 Mashujaa wataikaribisha Dodoma Jiji katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma
na Namungo dhidi ya Fountain Gate Uwanja wa Majaliwa, Lindi.
Ken Gold itacheza na Singida BS katika Uwanja wa
Sokoine, Mbeya Agosti 18 mwaka huu, JKT Tanzania wataialika Azam FC katika
dimba la Meja Jenerali Isamuhyo na Agosti 29, KMC itacheza na Coastal Union.
Mzunguko wa pili utaendelea Agosti 23, mwaka huu na
ratiba hiyo yenye timu 16 inatarajiwa kumalizika Mei 24 mwakani.
Wednesday, August 7, 2024
ZENA CHANDE, SOMOE NG'ITU WACHUKUA FOMU KUGOMBEA TWFA
Zena Chande |
Somoe ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa TWFA amechukua
fomu kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho wakati Zena ambaye ni Mjumbe
wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kutoka TWFA anawania
kutetea nafasi yake.
Zena ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari wa gazeti
la HabariLEO ni mzoefu katika nafasi mbalimbali za soka ikiwemo ikiwemo nafasi
ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
(TASWA) na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.
Kadhalika ni Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Soka la
Wanawake ya TFF hadi sasa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TWFA mkoa wa Dar
es Salaam.
Pia amewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Tuzo ya TFF
kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 na ni Kamishna wa Ligi Kuu Tanzania Bara hadi
sasa.
Kuhusu Somoe pia ni mwandishi wa habari wa gazeti la
Nipashe na Kamishna wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mwenyekiti wa TWFA Mkoa wa Dar
es Salaam na Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Soka la Wanawake ya TFF.
Katika taarifa iliyotolewa na Kamati ya uchaguzi huyo,
Makamu Mwenyekiti Benjamin Kalume alisema wagombea walianza kuchukua fomu leo na
mwisho ni Jumapili.
Pia alisema nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti,
Mwakilishi Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji
nafasi mbili.
“Mchujo utaanza Jumatatu Agosti 12 hadi 14 mwaka huu,
majina yatachapishwa Agosti 15-16 na kuweka pingamizi na kupokelewa ni Agosti
16-19,” alisema Kalume.
Aidha alisema kamati itapitia mapingamizi Agosti 20-22
na majina yatatangazwa na kubandikwa kwenye mbao za matangazo Agosti 23 na 24
mwaka huu.
Friday, July 26, 2024
Kokteli ya Jack Daniel’s na Coca-Cola katika kopo yazinduliwa Dar
Brown-Forman Corporation na Kampuni ya Coca-Cola wameingiza mtaani kitu kipya ambacho ni kileo kilicho tayari kwa kunywekwa (ARTD) .
Kinywaji hicho ambacho ni mchanganyiko wa Jack Daniel’s na Coca-Cola, ni kionjo kikamilifu cha kufurahia wakati mzuri na marafiki.
"Tunafurahi kuleta Jack Daniel’s na Coca-Cola kwenye soko la Afrika na kuwapa watumiaji njia mpya na ya kusisimua ya kufurahia mchanganyiko wa chapa zetu mbili za kipekee," alisema Peter Orfanidis, Meneja wa Kanda wa Brown-Forman.
"Tunapoendelea kusikiliza wateja kupitia bidhaa zetu mpya na kupanua upatikanaji wa Jack Daniel’s na Coca-Cola duniani kote, tunafurahi kuanzisha kinywaji hiki kilichohamasishwa na moja ya kokteili maarufu zaidi duniani.
"Bidhaa hii mpya inaonyesha kujitolea kwetu kuleta uzoefu bora wa ladha kwa watumiaji katika muundo rahisi wa kuwa tayari kunyweka," aliongeza Natasha Chetty, Mkurugenzi Mtendaji wa Bidhaa mpya katika kampouni ya Coca-Cola Afrika.
Kuingizwa mtaani kwa kinywaji hiki kunaonyesha dhamira ya dhati ya kampuni ya Coca-Cola ya kuwafanya wateja wake kuwa na furaha muda wote kwa kuwa na bunifu mbalimbali za kuwaburudisha.
Imeelekezwa kuwa baada ya kuzinduliwa kwa mafanikio katika masoko zaidi ya 25 duniani kote yakiwemo ya Marekani, Mexico, na Japan kinywaji cha Jack Daniel’s na Coca-Cola ARTD sasa kimefika Dar es salaam katika bara la Afrika.
Wataalamu wa vileo wamekiri kuwa ubunifu huu mpya utawapa watumiaji watu wazima wa Afrika fursa ya kufurahia ladha ya kipekee ya kokteili hii maarufu ya baa katika muundo rahisi wa kuwa tayari kunywekwa.
Uzinduzi ulijumuisha aina mbili za vinywaji yaani, Jack Daniel’s na Coca-Cola ya asili, na toleo la Coca-Cola Zero Sugar, ili kukidhi mapendeleo tofauti ya watumiaji.
Msemaji wa Coca-Cola Company akizungumza katika uzinduzi alisema kampuni yake inaelewa jukumu lake muhimu katika kukuza kunywa kwa uwajibikaji miongoni mwa wale waliofikisha umri wa kisheria wa kunywa, na itafuata Sera yake ya Uuzaji wa Pombe kwa Uwajibikaji inayoongoza katika sekta hiyo.
"Watumiaji wanaweza kutarajia kuona alama wazi za uwajibikaji kwenye kopo na ufungaji, ukisisitiza ujumbe kwamba kinywaji kinapaswa kufurahishwa kwa uwajibikaji na watu wazima tu waliofikisha umri wa kisheria wa kunywa," alisema.
Katika awamu ya kwanza baada ya uzinduzi kinywaji hicho kitapatikana katika maduka ya pombe na maeneo yaliyochaguliwa na itakuwa inapatikana katika makopo ya milimita 300 yenye kiwango cha pombe cha asilimia 5.
Wednesday, July 24, 2024
TIMU YA TAIFA YA MICHEZO YA OLIMPIKI UFARANSA 2024 YAWASILI PARIS
Kundi la kwanza la wachezaji wa Tanzania watakaoiwakilisha nchi katika Michezo ya Olimpiki limewasili salama asubuhi ya leo Julai 24, 2024 jijini Paris nchini Ufaransa.
Kundi hilo la kwanza lina waogeleaji wawili, Sofia Anisa Latiff na Collins Phillip Saiboko na mwalimu wao Alexander Harrison Mwaipasi pamoja na Daktari wa timu, Dkt Eliasa Abdallah Mkongo.
Waogeleaji wataanza kuchuana Agosti 30 mwaka huu, ambapo Collins Phillip Saiboko atashindana katika michuano ya mita 100 Freestyle kwa wanaume huku, Sofia Anisa Latiff atashindana Agosti 3, katika mita 50 freestyle kwa wanawake.
Mwingine aliyewasili leo Paris ni mwalimu wa mchezo wa Judo, Innocent John Mallya, ambaye mchezaji wake, Andrew Thomas Mlugu (Kg 73), tayari yupo Paris kwa mwaka mmoja katika kambi maalumu ya mazoezi ya CRJ Centre iliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) na ataanza kuingia dimbani Agosti 2 mwaka huu.
Wanamichezo wanne, ambao wote ni wakimbiaji wa Marathon, bado wako kambini Jijini Arusha wakiendelea kujifua na wanatarajiwa kuwasili Paris Augosti 7 na Marathon itakuwa Agosti 11, 2024.
Wanariadha hao wa marathon ni wanaume Alphonce Felix Simbu na Gabriel Geay, na wanawake ni Jackline Juma Sakilu na Magdalena Crispin Shauri.
KCB EAST AFRICA GOLF TOUR KUFANYIKA LUGALO
SHINDANO la wazi la mchezo wa gofu (KCB EAST Africa
Golf tour) linatarajiwa kufanyika Agosti 3 mwaka huu katika Viwanja vya Lugalo
Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa klabu ya
Lugalo, Brigedia Jenerali mstaafu, Michael Luwongo alisema shindano hilo
litashirikisha wachezaji 150 kutoka nchi mbalimbali na klabu za hapa nchini.
Luwongo alisema lengo ni kupata timu ya wachezaji
wanne watakaokwenda kushiriki mashindano Nairobi, Kenya Desemba 6 mwaka huu.
"Maandalizi ya shindano hili yanaendelea vizuri,
mpaka sasa tunaendelea kuboresha miundombinu ya viwanja vyetu ili shindano
lifanyike kwa weledi” alisema Luwongo.
Pia aliipongeza Benki ya KCB kwa udhamini wao na
kuwataka wale ambao hawajathibitisha ushiriki wao wafanye haraka muda umeisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa KCB, Cosmas Kimario
alisema benki hiyo inatoa huduma kwa jamii pamoja na michezo mbalimbali ikiwemo
riadha, mpira wa miguu na ngumi.
"Tuna uhakika hii timu itakayokwenda Kenya
itafanya vizuri na kurudi na ushindi nyumbani, ili fainali ijayo ifanyika hapa
nchini, alisema Kimario.
Alisema wameamua kuwekeza katika michezo kwa lengo la
kukuza vipaji vya vijana wadogo wanaochipukia.
Naye nahodha wa klabu ya Lugalo, Meja Japhet Masai
alisema shindano hilo litachezwa kwa mfumo wa kuhesabu mashimo kwa pointi na atakayepata
pointi nyingi atapata nafasi ya kwenda Kenya.