TANZANIA ITAJENGWA NA WATANZANIA: WAZIRI SANGU AWAGUSA DIASPORA SAUDI ARABIA, AWAHIMIZA KULETA MITAJI NYUMBANI



Kauli mbiu ya Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe imechukua sura mpya na ya kipekee nchini Saudi Arabia baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mheshimiwa Deus Sangu, kutoa wito mzito kwa Watanzania waishio ughaibuni kuwa sehemu ya injini ya maendeleo ya taifa lao. 

Akiwa katika ziara ya kikazi nchini humo, Waziri Sangu amewasisitiza Diaspora kuitazama Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kama dira yao binafsi itakayowaongoza kubaini fursa za uwekezaji na kuchangia katika kukuza uchumi wa nyumbani.

Katika mazungumzo yake na Watanzania waishio Saudi Arabia, Waziri Sangu ameweka bayana kuwa, kuwa mbali na nyumbani hakupunguzi haki wala wajibu wa mwananchi kuwasaidia ndugu, jamaa, na jamii inayomzunguka nchini Tanzania. 

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetengeneza mazingira rafiki na wezeshi ya uwekezaji, hivyo ni wakati muafaka kwa Diaspora kuacha kutumia mitaji yao nje pekee na badala yake waelekeze rasilimali hizo nyumbani ambako kuna uhakika wa usalama na faida.

Waziri Sangu amesisitiza kuwa mchango wa Diaspora si tu kutuma fedha za matumizi ya kila siku kwa familia, bali ni kuleta mitaji mikubwa, utaalamu, na teknolojia ambayo itazalisha ajira kwa vijana na kuimarisha soko la ajira nchini. 

Amewakumbusha kuwa mazingira ya biashara nchini Tanzania yameboreshwa kwa kiasi kikubwa, na Serikali ipo tayari kuwapokea na kuwapa ushirikiano wa hali ya juu wale wote watakaoamua kuanzisha miradi ya maendeleo kuanzia viwanda, kilimo biashara, hadi sekta ya huduma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Diaspora nchini Saudi Arabia, Dkt. Zidikheri Msechu, ameeleza kuwa Watanzania waishio huko wameguswa na wito huo na wako tayari kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. 

Amesema kuwa wana hamu ya kuona rasilimali walizozipata ughaibuni zikileta mabadiliko chanya nyumbani, huku akiahidi kuwa watakuwa mabalozi wa kuitangaza Tanzania kama kitovu bora cha uwekezaji barani Afrika.

Ziara hii ya Waziri Sangu, inayojumuisha ushiriki wake katika Mkutano wa Mawaziri wa Kazi Duniani, inatoa ujumbe  kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa kila Mtanzania, popote alipo duniani. Ni imani ya Serikali kuwa endapo Diaspora wataielewa vema Dira ya 2050 na kuamua kuwekeza nyumbani, safari ya kuelekea uchumi wa juu itakuwa fupi na yenye mafanikio makubwa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments