KIZAAZAA CHA WAANDISHI ELIMU YA KUSHUGHULIKIA WAATHIRIKA WA MAJANGA
Tukio la hivi karibuni mkoani Dar es Salaam, ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani, Jaji Mkuu Mstaafu Profesa Ibrahim Juma, aliwaomba waandishi wa habari kutoka nje ya ukumbi wa mkutano, limeibua mjadala mzito kuhusu mipaka ya habari na haki ya faragha kwa waathirika wa majanga.
Hatua hiyo iliyochukuliwa katika ukumbi wa Wilaya ya Ubungo, Januari 24, 2026, si tu amri ya kisheria, bali ni funzo la kimaadili kwa tasnia ya habari nchini.
Profesa Juma alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi waliogubikwa na hofu kuwa usiri wao unavunjwa. Katika mazingira ya migogoro ya kisiasa au kijamii, mwathirika anahitaji nafasi salama (Safe Space) ya kuelezea maumivu yake bila hofu ya kurekodiwa au kuonekana kwenye vyombo vya habari, jambo ambalo linaweza kumletea madhara zaidi ya kisaikolojia au kijamii.
Faragha dhidi ya Haki ya Kuhabarisha
Uandishi wa habari una dhima kuu ya kuhabarisha umma, lakini dhima hiyo hupata kikwazo pale inapokutana na "Haki ya Utu na Faragha" ya mwathirika. Profesa Juma amesisitiza kuwa ili Tume ipate ukweli wa mambo yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ni lazima wananchi wawe na uhuru kamili wa kuongea.
Wataalamu wa maadili ya habari wanaeleza kuwa majeraha ya uvunjifu wa amani mara nyingi huambatana na aibu, hofu, na msongo wa mawazo (PTSD). Waandishi wa habari wanapokumbatia kamera na vinasa sauti mbele ya watu waliojeruhiwa kisaikolojia, wanaweza kugeuka kuwa "chanzo cha maumivu mapya" badala ya kuwa wasaidizi wa kurekebisha hali. Hapa ndipo hitaji la "dozi ya elimu" ya faragha linapokuwa muhimu kwa mwanahabari wa karne ya 21.
Kovu la Saikolojia kwa Watoto na Jamii
Mbali na usiri, mkutano wa Ubungo umeibua upande mwingine wa majanga: Athari za kisaikolojia kwa watoto. Mashuhuda kama John Ndunguru wameeleza jinsi watoto wao wanavyopata mshtuko hata wanaposikia sauti ya pikipiki, ikiwa ni matokeo ya kushuhudia matukio ya barabarani wakati wa machafuko.
Mmomonyoko wa Maadili na Hitaji la Sheria
Kwa upande mwingine, sauti za wadau kama Ali Mwombeki, mfanyabiashara aliyevunjiwa maduka yake, zinashauri kurejeshwa kwa misingi ya dini na maadili shuleni. Mwombeki anahoji kuwa vijana waliohusika katika uvunjifu wa amani ni zao la mmomonyoko wa maadili. Pendekezo lake la kufanya somo la dini kuwa la lazima na kutoa adhabu kali kwa vijana wahalifu ni kilio cha jamii inayotaka nidhamu irejee.
Wakati Tume hiyo ikiwa imeshatembelea mikoa minane na kuhitimisha Dar es Salaam, ujumbe ni mmoja: Tanzania inataka kupona. Lakini uponyaji huo hauwezi kukamilika kama waandishi wa habari hawatatambua mipaka yao, na kama mfumo wa elimu hautashughulikia afya ya akili ya kizazi kilichoshuhudia majanga haya.
Kauli ya Jaji Mkuu Mstaafu Profesa Juma ni kengele ya kuamsha tasnia ya habari. Ni lazima waandishi wajifunze uandishi wenye "utu" (Humanitarian Journalism) unaozingatia faragha ya mwathirika kuliko "Breaking News." Kama nchi, ni lazima tuchunguze si tu kilichotokea Oktoba 29, bali pia jinsi ya kuandaa jamii inayojua thamani ya usalama, maadili, na staha kwa mwingine.

Post a Comment