CCM yamteua Dk Komba kumrithi Jenista, Makonda na Lusinde waingia NEC ya CCM
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imemteua Dk Lazaro Komba kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Peramiho.
Dk Komba aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa alishika nafasi ya tano katika kura za maoni kwa kupata kura 213 na amewahi kugombea mara kadhaa ubunge wa jimbo hilo.
Uamuzi huo wa Kamati Kuu ya CCM, unamuondoa Victor Mhagama aliyeongoza kwa kura 3,040 katika mbio za kurithi nafasi hiyo iliyoachwa wazi na mama yake, Jenista Mhagama aliyefariki dunia Desemba 11, 2025 akiwa Mbunge wa Peramiho kwa miaka 20.
Uteuzi wa Dk Komba umefanyika chini ya Ibara ya 105 (7)(f) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la Julai 2025.
Katika kikao hicho kilichofanyika jana Unguja chini ya Uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan,Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda na Livingstone Lusinde Mbunge wa Mtera na Naibu Waziri wa Kilimo wameteuliwa kuwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa kwa upande wa wanaume na kwa wanawake ni Asia Halamga ambaye ni mbunge wa kuteuliwa.
Kwa upande wa Zanzibar walioteuliwa ni Khamis Musa Omar na Tauhida Cassian Galos.
Agness Hokororo ameteuliwa kuwa katibu wa wabunge wa CCM wakati wenyeviti ni Najima Murtaza, Deodatus Mwanyika na Cecilia Pareso.
Aidha Kamati Kuu hiyo imefanya uteuzi wa uongozi wa CCM wanaotokana na Baraza la Wawakilishi ambao ni Said Ali Juma, Hamza Hassan Juma na Lela Mohamed Mussa.
Wawakilishi wa CCM watakaoingia bungeni kwa mujibu wa Katiba ni Bakar Hamad Bakar, Dk Shaame Ali Ali, Simai Mohamed Said na Fatma Ramadhan Mandoba.
Machano Othman Said ameteuliwa kuwa katibu wa wawakilishi wote wa CCM na Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi ni Mahmoud Omar Hamad na Hudhaima Mbarak Tahir.
Mwisho

Post a Comment