Sinners Yatikisa Tuzo za Oscar: Ryan Coogler Aweka Rekodi ya Kihistoria
Pazia la kinyang'anyiro cha tuzo za 98 za Academy, maarufu kama Oscar, limefunguliwa huku filamu ya kutisha kuhusu majini (vampires) iitwayo Sinners ya mwongozaji Ryan Coogler ikizua taharuki ya kihistoria.
Filamu hiyo imefanikiwa kupata uteuzi katika vipengele 16, ikiwemo Filamu Bora, Mwongozaji Bora, Muigizaji Bora wa Kiume, na Mswada Bora wa Awali.
Hatua hii ni ya kipekee kwani filamu za kutisha mara nyingi zimekuwa hazipenyi Academy, lakini zaidi ni kwa sababu hakuna filamu iliyowahi kufikisha uteuzi zaidi ya 14 katika historia, rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na filamu za All About Eve (1950), Titanic (1997), na La La Land (2016).
Wakosoaji wa filamu wanasema Sinners ni kazi ya sanaa inayozungumzia muziki wa blues kama kiunganishi cha kichawi kati ya walimwengu na nyakati tofauti. Coogler amefanikiwa kuonyesha kuwa muziki huu si tu kumbukumbu ya uthabiti wa watu weusi baada ya utumwa, bali pia ni kimbilio la baadaye. Kupitia filamu hii, Coogler ametoa mtazamo mpya wa kisiasa kuhusu viumbe hawa wa kufikirika na kuifanya kuwa moja ya kazi bora zaidi za mwaka 2025.
Hata hivyo, Sinners siyo peke yake inayowindwa na tuzo hizo. Filamu ya vichekesho na siasa ya Paul Thomas Anderson (PTA) iitwayo One Battle After Another inafuatia kwa ukaribu ikiwa na uteuzi katika vipengele 13. Filamu hii tayari imeanza kuonyesha makucha baada ya kung'ara kwenye tuzo za Golden Globes mapema mwezi huu, na wengi wanaipa nafasi kubwa ya kunyakua tuzo ya Filamu Bora na Mwongozaji Bora. Licha ya Paul Thomas Anderson kuwa na uteuzi 11 huko nyuma kupitia filamu kama There Will Be Blood, bado hajawahi kushinda Oscar hata moja.
Filamu hizi mbili, ambazo zote zimetayarishwa na kampuni ya Warner Bros., zimeipa studio hiyo jumla ya uteuzi 29, mafanikio makubwa zaidi katika historia ya miaka 102 ya studio hiyo. Haya yanatokea wakati Warner Bros. ikijiandaa kuuzwa kwa kampuni ya Netflix kwa thamani ya dola bilioni 72, hatua inayowatia wasiwasi wapenzi wa sinema kuhusu mustakabali wa kuonyesha filamu kwanza kwenye kumbi za sinema kabla ya mtandaoni.
Kwa upande mwingine, Netflix imepata mafanikio kupitia filamu ya Guillermo del Toro ya Frankenstein iliyopata uteuzi tisa, ikilingana na drama ya Marty Supreme ya Josh Safdie na Sentimental Value ya Joachim Trier. Filamu za kimataifa pia zimeleta mshangao mwaka huu, ambapo The Secret Agent ya Brazil na Sentimental Value ya Norway zimepata uteuzi wa Filamu Bora pia, jambo ambalo si la kawaida.
Ushindani mkali unatarajiwa katika kipengele cha Muigizaji Bora wa Kiume, ambapo kijana Timothée Chalamet kupitia Marty Supreme atachuana na mkongwe Leonardo DiCaprio wa One Battle After Another. Wengine katika orodha hiyo ni pamoja na Ethan Hawke, Michael B. Jordan, na Wagner Moura aliyeshinda tuzo ya Golden Globe hivi karibuni. Katika upande wa wanawake, ushindani mkali uko kati ya Jessie Buckley na Rose Byrne, wakikabiliana na mshindi wa mara mbili Emma Stone pamoja na Renate Reinsve na Kate Hudson.
Mshangao mwingine wa mwaka huu ni kutupwa nje kwa filamu ya Wicked: For Good, ambayo ilitarajiwa kufanya vizuri lakini imekosa uteuzi katika vipengele muhimu kama Muigizaji Bora wa Kike na Filamu Bora. Mashabiki wa Ariana Grande na Cynthia Erivo wamebaki na maswali mengi baada ya tangazo hilo. Tuzo hizi za 98 za Oscar zitafanyika Jumapili, Machi 15 katika ukumbi wa Dolby Theatre mjini Los Angeles, zikiongozwa na Conan O’Brien.
Post a Comment