Bandari ya Dar es Salaam: haijauzwa imekodishwa kwa tija




Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Gerson Msigwa, ametoa ufafanuzi mzito na wa kina mbele ya vyombo vya habari leo katika Bandari ya Dar es Salaam, akiondoa mkanganyiko wowote kuhusu umiliki wa lango hilo kuu la uchumi wa Tanzania. 

Katika hotuba yake iliyosheheni data za kiufundi, Msigwa amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haijauza bandari hiyo, bali imeingia mikataba ya upangishaji na uendeshaji kwa miaka 33 na kampuni zenye uzoefu mkubwa wa kimataifa ambazo ni DP World na Adani  ili kuiongezea tija. 

Amesema kampuni hizo kubwa zimeanzisha kampuni tanzu zilizosajili nchini na zinazofuata sheria za hapa nchini kwa ajili ya kuhjudumia bandari hiyo.

Ndugu Msigwa alifafanua kuwa lengo kuu la Serikali katika uamuzi huu ni kupunguza mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji uliokuwa unaikabili Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na badala yake kuvuna mapato ya uhakika kupitia kodi na ada za upangishaji huku ufanisi ukiongezeka.

Uchambuzi wa kina unaonesha kuwa kampuni hizi tayari zimeanza kumwaga mabilioni ya fedha katika maboresho ya miundombinu, ambapo DP World pekee imeshawekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 214.2 hadi kufikia Juni 2025 kwa ajili ya kununua mitambo mipya na kusanifu mifumo ya kisasa ya TEHAMA. 

Kwa upande wao, kampuni ya TEAGTL inayomilikiwa na Adani inaendelea na uwekezaji wa Shilingi Bilioni 410.4 unaohusisha ukarabati wa miundombinu ya kuhifadhi makasha na uboreshaji wa gati namba 8 hadi 11, ikiwemo kuongeza urefu wa gati kwa mita mia moja. 

Matunda ya uwekezaji huu tayari yameanza kuonekana ambapo gharama za uendeshaji wa bandari zimepungua kwa wastani wa asilimia 57, jambo linaloimarisha uwiano wa faida kwa TPA kufikia wastani wa asilimia 78, huku nchi ikizidi kunufaika na kodi za forodha zilizopaa hadi Shilingi trilioni 12.33 katika mwaka wa fedha 2024/25.

Msigwa alisema kwamba Serikali inajivunia ufanisi mkubwa uliopatikana kutokana na uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa Kampuni ya DP World na Adani ambapo uwekezaji huo umepaisha makusanyo kwa asilimia 17.

No comments