RAIS DKT. SAMIA KUONGOZA ZOEZI LA UPANDAJI MITI ZANZIBAR KUADHIMISHA SIKU YAKE YA KUZALIWA




 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza zoezi maalum la upandaji miti litakalofanyika tarehe 27 Januari, 2026, katika maeneo ya Bungi Kilimo na Kizimkazi, Zanzibar. Hatua hiyo ni sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, ambapo zoezi hilo limebeba kaulimbiu isemayo “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti”.

Tukio hilo linaakisi dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais katika kuendeleza ajenda ya Taifa ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Zoezi hilo linalenga kuimarisha ulinzi wa vyanzo vya maji, kukuza uoto wa asili, na kuchangia juhudi za kivitendo za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.

Mheshimiwa Rais ametoa wito kwa Watanzania wote kujenga utamaduni wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa hiari. Amesisitiza kuwa ulinzi wa mazingira ni msingi mkuu wa uhai, maendeleo, na usalama wa Taifa, huku akibainisha kuwa zoezi hilo ni ishara ya uwajibikaji wa pamoja kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais kupitia kwa Mkurugenzi wake, Bakari S. Machumu, imewahimiza wananchi, taasisi, na wadau wa mazingira kuunga mkono dhamira hiyo ya Rais. Wananchi wamehimizwa kuendeleza ajenda ya uhifadhi kwa kupanda angalau mti mmoja katika maeneo ya nyumbani, shuleni, kazini, au maeneo mengine ya jamii.


No comments