MPOGOLO AHIMIZA UZALENDO KWA KUPANDA MITI ILALA
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuonyesha uzalendo wa kweli kwa kuitikia wito wa utunza mazingira kupitia upandaji wa miti katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mpogolo ametoa kauli hiyo Januari 27,2026, wakati wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, yaliyofanyika katika shule ya wasichana Jangwani jijini hapa.
Akizungumza na hadhara katika shule hiyo, Mkuu wa Wilaya amebainisha kuwa uzalendo wa dhati unapaswa kuanzia katika vitendo vinavyolinda rasilimali za taifa ambapo mazingira ni kipaumbele kikubwa.
Amesema kuwa Rais Samia amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nchi inakuwa ya kijani, hivyo wananchi wanapaswa kufuata maono hayo kwa vitendo ili kuweka msingi imara wa maisha bora kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Katika kutilia mkazo agizo hilo, Mheshimiwa Mpogolo ametoa wito kwa wananchi wa Ilala kuhakikisha kila kaya inapanda miti isiyopungua mitatu. Aidha, amewaelekeza wakuu wa shule na viongozi wa taasisi mbalimbali kusimamia ipasavyo utunzaji wa miti inayopandwa ili kuhakikisha inastawi na kuleta tija iliyokusudiwa badala ya kuishia kupanda bila ufuatiliaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya, amesema kuwa halmashauri imejipanga kikamilifu kutekeleza kaulimbiu inayosema uzalendo ni kutunza mazingira. Amesema kuwa mkakati uliopo ni kupanda zaidi ya miti milioni moja katika maeneo mbalimbali ya jiji, huku wakisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza uharibifu wa misitu.
Maadhimisho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo lililotolewa na Ofisi ya Ikulu iliyoelekeza jamii kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais Samia kwa kufanya shughuli za kijamii zinazogusa mazingira moja kwa moja, ikiwa ni ishara ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Post a Comment