Uwekezaji katika Michezo chachu ya maendeleo nchini

 




WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Maendeleo ya michezo yamechangiwa na juhudi kubwa za viongozi wakuu wa nchi Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambao wameweka vipaumbele katika sekta hiyo.

Amezungumza hayo Januari 24, 2026 wakati akifunga Mashidano ya mpira wa Pete ya Kombe la Muungano Zanzibar ambapo timu ya KVZ imeibuka bingwa baada ya kushinda michezo yote 10.

"Kupitia mpango wa "Goli la Mama", tumeshuhudia ongezeko la Bajeti, ujenzi wa viwanja vipya na mazingira bora kwa wanamichezo wetu, matokeo ya jitihada hizi ni wazi na tumeshuhudia Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ‘Taifa stars’ imefika hadi hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON pale Morocco na ni kwa mara ya kwanza tangu kuanza kushiriki mashindano hayo," amesema Mhe. Masauni.

Amesema ujenzi pamoja na uboreshaji wa Viwanja vya michezo vimewezesha mashindano mbalimbali kufanyika yakiwemo mashindano ya CHAN yaliyohusisha nchi za Kenya, Uganda na Tanzania. Huu ni ushahidi kuwa Tanzania, kupitia Muungano wake, inainuka kisoka Afrika na Duniani.






Ameeleza Maendeleo haya yamewekewa chachu ya ushirikiano kati ya serikali zetu mbili chini ya wizara husika za michezo na taasisi zetu za ZFF, TFF, CHANEZA NA CHANETA ambazo zinasimamia michezo hii ya mpira wa miguu na Pete kwa weledi mkubwa sana.

“Nawapongeza viongozi wa wizara hizi na wasaidizi wao pamoja na viongozi wa ZFF, TFF, CHANEZA NA CHANETA kwa kuhakikisha wanasimamia maendeleo ya michezo nchini," ameongeza Masauni.

Aidha katika hatua ingine Waziri Masauni amewashukuru waandaji wa Mashindano haya CHANEZA na CHANETA na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutekeleza agizo la Rais la kuimarisha Muungano kupitia michezo alilolitoa Aprili 13, 2024 wakati akipokea taarifa ya Kamati Maalum iliyowasilisha maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHANEZA Bi. Nasra Juma ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa  kushiriki na kudhamini mashindano hayo ambayo yamekuwa ya ushindani mkubwa.

Amesema mashindano hayo ni muhimu kwa kuwa yamekuwa yakitoa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano makubwa kwa Bara la Afrika na jumuiya ya Afrika Mashariki. Mashindano haya yalishirikisha timu 11, tano kutoka Zanzibar na sita kutoka Tanzania Bara.

No comments