MAPAFU YA AJIRA YANAVYOPUMUA: SIKU 100 ZA RAIS SAMIA MAENEO MAPYA YA VIWANDA MIKOA 11
Katika kipindi cha siku 100 za kwanza tangu kuanza kwa muhula mpya wa uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya Uchaguzi Mkuu, sekta ya viwanda na biashara nchini imepata msisimko wa kipekee ambao umeanza kufungua milango ya ajira kwa maelfu ya vijana.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameanika mafanikio hayo kumi na mawili (12) ambayo yanatajwa kama "mapafu ya ajira" yanayopumua kwa nguvu, yakichangiwa na uwekezaji mkubwa, ujenzi wa mitaa ya viwanda, na programu mahususi za kuwawezesha vijana kibiashara.
Moja ya mafanikio makubwa yaliyotajwa ni uwezo wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kuvutia wawekezaji wakubwa katika Kongani ya Viwanda ya Tamko. Waziri Kapinga amebainisha kuwa mwekezaji Goodlife Investment Tanzania anatarajiwa kuanza rasmi uunganishaji wa magari ya umeme nchini.
Mradi huu utakaotekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 17,460, hauleti tu teknolojia mpya, bali unatarajiwa kuzalisha mamia ya ajira za kiufundi kwa vijana wa Kitanzania, huku ukiweka nchi katika ramani ya mataifa yanayotumia nishati safi.
Ajira 100,000 kwa Vijana: Programu ya TISEZA na SIDO
Katika hatua ya kijasiri ya kupambana na ukosefu wa ajira, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA) pamoja na SIDO, imeanzisha programu maalumu inayolenga kuwezesha biashara 100,000 zinazoongozwa na vijana.
Programu hii si ya maneno tu; tayari maeneo maalumu ya viwanda vya vijana yametengwa katika mikoa ya kimkakati:Dar es Salaam (Kigamboni);Mwanza (Nyakato);Arusha (Azimio);Mbeya (Songwe);Kigoma (Uvinza) Na Ruvuma (Nyasa).
Waziri Kapinga amefafanua kuwa maeneo manne ya SIDO katika mikoa ya Kigoma, Morogoro, Mbeya, na Singida yapo tayari kwa uzinduzi, hatua itakayozalisha ajira za moja kwa moja 4,619, nyingi zikiwa ni kwa ajili ya vijana.
Sekta ya kilimo pia imeguswa na mapinduzi haya ya siku 100. Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO) imekamilisha ujenzi wa viwanda vitatu vya kuongeza thamani mazao ya kilimo ambavyo tayari vimeanza uzalishaji kibiashara.
Aidha, kiwanda cha nne kinatarajiwa kukamilika Februari 2026. Viwanda hivi vinatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa vijana zaidi ya 300 na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 700, huku vikihakikisha mkulima anapata soko la uhakika na bei nzuri kwa mazao yake.
Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Viwanda (TIRDO) imeingia mguu na mguu kwenye utafiti wa madini ya kimkakati. Tayari utafiti wa kina umeanza katika wilaya za Kyerwa (Kagera) na Ikungi (Singida).
Lengo ni kuhakikisha rasilimali hizi zinachimbwa kwa usalama na kuongezwa thamani hapa nchini. Hatua hii imetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha biashara ndogondogo na uhamisho wa teknolojia kwa wananchi wa maeneo husika, huku ikiweka misingi ya uwekezaji mkubwa wa viwanda vya madini.
Siku 100 za Rais Samia zimeonyesha kuwa serikali imejikita katika vitendo zaidi kuliko maneno. Kwa kufungua maeneo mapya ya viwanda katika mikoa 11 na kuweka mifumo rafiki ya mitaji, "mapafu ya ajira" nchini sasa yanapumua kwa kasi, yakitoa matumaini mapya kwa vijana na kuimarisha uchumi wa viwanda.
Post a Comment