MAREKEBISHO MAKUBWA SEKTA YA AFYA: SERIKALI SASA YAWEKEZA KWENYE HUDUMA, TEKNOLOJIA
Serikali ya Awamu ya Sita imetangaza mwelekeo mpya wa utendaji katika sekta ya afya nchini, ikihama rasmi kutoka katika sifa ya ujenzi wa miundombinu ya majengo pekee na kuelekeza nguvu zake zote katika kuboresha miundombinu ya huduma bora kwa mwananchi kupitia teknolojia na ubunifu.
Hatua hiyo imebainishwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati wa uzinduzi wa mfumo mpya wa kidijitali wa Ongea na Waziri wa Afya uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha, ambapo amesisitiza kuwa taifa la kisasa haliwezi kupimwa kwa uzuri wa barabara na majengo marefu ikiwa wananchi wake bado wanataabika kupata huduma za msingi za afya.
Mwelekeo huu unadhihirisha azma ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye majengo ya hospitali nchi nzima sasa unaendana na thamani ya huduma wanazopata wananchi.
Waziri Mchengerwa ameweka wazi kuwa zama za kuongoza sekta hiyo kwa kubahatisha zimefikia kikomo na sasa wizara hiyo inaingia katika zama za kuongoza kwa kutumia ushahidi wa kisayansi na takwimu.
Kupitia mfumo huu wa kidijitali, serikali inalenga kuvunja urasimu uliokuwa ukiwakuta wananchi mahospitalini, ikiwemo kero ya foleni ndefu, ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu upatikanaji wa dawa, na changamoto za mifumo ya rufaa ambazo zimekuwa zikizorotesha ustawi wa jamii.
Katika kutilia mkazo mageuzi hayo, serikali imetoa wito maalumu kwa vijana wabunifu nchini kuchangamkia fursa ya kuleta suluhu za kiteknolojia zitakazosaidia kuimarisha mifumo ya afya.
Waziri amesisitiza kuwa ubunifu wa vijana ndio utakaokuwa injini ya mabadiliko haya, ukilenga kupunguza makosa ya kitaalamu na kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali yao.
Uzinduzi wa mfumo wa Ongea na Waziri ni hatua ya kimkakati inayompa mwananchi sauti ya moja kwa moja ya kutoa mrejesho kuhusu huduma anazopata.
Hatua hii si tu inaongeza uwazi na uwajibikaji kwa watumishi wa afya, bali pia inaiwezesha wizara kufanya maamuzi yenye tija kulingana na mahitaji halisi ya wananchi.

Post a Comment