Serikali yaimarisha uratibu maandalizi ya AFCON 2027
Serikali imeendelea
kuimarisha uratibu wa maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika
(AFCON 2027) yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.
Katika
kuhakikisha kila kitu kinakwenda kwa wakati, wizara na taasisi mbalimbali za
serikali zimekutana jijini Dar es Salaam kujadili hatua iliyofikiwa na kuweka
mikakati thabiti ya kukamilisha maandalizi yote yanayohitajika.
Kikao
hicho kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,
Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk. Jim Yonazi, kilikutanisha makatibu wakuu wa
wizara pamoja na watendaji wakuu wa taasisi za serikali.
Katika
majadiliano hayo, maeneo kuu yaliyochambuliwa ni pamoja na maendeleo ya
utekelezaji wa miradi ya miundombinu, uboreshaji wa bajeti, uratibu wa shughuli
mbalimbali, pamoja na tathmini ya changamoto zilizojitokeza na hatua za haraka
za kuzitatua.
Mashindano
hayo ya AFCON 2027 yanaandaliwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Kenya na
Uganda, ambapo kwa upande wa Tanzania inatarajiwa kutumia vituo vya Dar es
Salaam, Arusha na Zanzibar.
Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na taasisi zingine,
serikali inaendelea kuratibu miradi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya
mashindano, viwanja vya mazoezi, barabara na miundombinu mingine wezeshi ili
kuhakikisha nchi ipo tayari kuwapokea wageni na timu zitakazoshiriki.

Post a Comment