Britney Spears miaka mitano bila usimamizi wa baba yake

 



Tangu Mahakama ilipoweka huru dhidi ya usimamizi tarehe 12 Novemba 2021, mwanamuziki nguli wa muziki wa Pop, Britney Spears, ameweka wazi jambo moja kuu kwamba yeye ni binadamu wa kawaida na ana udhaifu wake.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita haikuwa rahisi kwa mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 44, kwani amepitia ndoa, talaka, kupoteza mimba, lakini pia ameweza kupaza sauti yake kupitia kitabu chake kilichouza sana pamoja na nyimbo zake mpya.

Spears mwaka huu alikamatwa kwa kuendesha gari akiwa amelewa pamoja na kukaa kwenye kituo cha marekebisho ya tabia.

Pamoja na changamoto hizo zote, amekuwa kwenye juhudi kubwa za kujenga upya uhusiano wake na wanae.

Vyanzo vya karibu vinaripoti kuwa pamoja na vichwa vya habari vinmavyokera, Spears hivi sasa anaishi maisha ya utulivu mkubwa nyumbani kwake ambapo burudani yake kubwa ni kucheza muziki na kurekodi video za Instagram ambazo zinamsaidia kama tiba ya nafsi.

Mfumo Mpya

Mitandao ya kijamii imekuwa njia kuu ya Britney kuwasiliana na mamilioni ya mashabiki wake duniani. Badala ya kutumia mahojiano ya televisheni au muziki kama zamani, sasa hivi anatumia video anazojirekodi mwenyewe akiwa sebuleni kwake huko Thousand Oaks, California, kueleza hisia zake na kuongelea maumivu ya miaka 13 aliyokaa chini ya usimamizi wa baba yake, Jamie Spears.

Pia, kando na hayo, msanii huyo anawashirikisha mashabiki wake picha za wanaye, Sean Preston mwenye umri wa miaka 21 na Jayden James mwenye umri wa miaka 20. Baada ya kukaa mbali kwa muda mrefu ambapo wanaye hao walihamia Hawaii na baba yao Kevin Federline mwaka 2023, sasa wamerejea Los Angeles na wanatenga muda mwingi kukaa na mama yao.

Britney anahisi anafidia muda uliopotea na anafurahi kuona vijana wake wakifanya vizuri kwenye tasnia ya mitindo na muziki.

Kulinda Heshima

Tangu kumalizika kwa usimamizi wa kisheria dhidi yake, Britney amesisitiza mara kadhaa kuwa amestaafu kufanya muziki wa jukwaani na hataki tena kutumbuiza nchini Marekani. Kutokana na msimamo huo, timu yake ya usimamizi imejikita zaidi katika kulinda na kusherehekea heshima ya kazi alizofanya miaka ya nyuma badala ya kumlazimisha kutoa nyimbo mpya.

Hivi karibuni, kampuni iliyonunua haki za nyimbo zake kwa takriban dola milioni 200 imekuwa ikitumia nyimbo zake za zamani kwenye matangazo makubwa ya biashara na maonyesho ya mitindo duniani. Wasaidizi wake bado wana matumaini kuwa siku moja anaweza kutamani kurudi jukwaani, ingawa kwa sasa amekuwa akiimba tu kwa furaha zake binafsi akiwa nyumbani au kwenye gari anapokuwa na wanae.

Changamoto



Mwaka huu umekuwa na mawimbi makubwa kwa msanii huyo baada ya kukamatwa mwezi Machi kwa tuhuma za kuendesha gari akiwa amelewa. Matukio hayo yaliwasukuma wanae wa kiume, Preston na Jayden, kukaa naye chini na kumsihi atafute msaada wa kisaikolojia na matibabu ya kitaalamu.

Kufuatia ushauri wa wanae, Britney alijiunga na vikundi vya ushauri nasaha na baadaye kujipeleka mwenyewe kwenye kituo cha mapumziko na matibabu huko Maine. Baada ya kurejea, alifikia makubaliano na waendesha mashitaka kwa kukiri kosa dogo la kuendesha gari kwa hatari, ambapo alipewa kifungo cha nje cha mwaka mmoja na amri ya kumwona daktari wa saikolojia mara kwa mara ili kuimarisha afya yake ya akili na mfumo wa maisha.

Migogoro ya kifamilia

Wakati uhusiano wake na wanawe ukizidi kuwa imara, uhusiano kati ya Britney na familia yake ya kuzaliwa bado haujatengamaa. Britney haongei kabisa na baba yake Jamie Spears na ameweka wazi kuwa hatamsamehe kamwe kwa jinsi alivyomfanyia wakati wa usimamizi, ingawa anafahamu kuhusu changamoto za kiafya zinazomkabili baba yake huyo kwa sasa.

Uhusiano wake na mama yake Lynne Spears bado nao wa kusuasua kutokana na ukosefu wa uaminifu, ingawa mara chache huwa wanawasiliana na kuonana.

Kwa upande wa mdogo wake wa kike, Jamie Lynn Spears, Britney ameendelea kumtupia lawama kwenye mitandao ya kijamii kuhusu matukio ya nyuma, huku mawasiliano yao yakibaki kuwa ya ujumbe mfupi pekee. Ndugu pekee wa familia yake anayeelezwa kuwa karibu naye na anayemwamini ni kaka yake mkubwa Bryan Spears.

Maisha ya Mapenzi



Katika upande wa mahusiano ya kimapenzi, Britney amechagua kubaki peke yake kwa sasa. Baada ya ndoa yake ya miezi 14 na Sam Asghari kuvunjika mwezi Agosti 2023, na baadaye kuwa kwenye mahusiano ya kusuasua na mfanyakazi wake wa zamani Paul Richard Soliz hadi walipoachana mapema mwaka jana, Britney hajaingia tena kwenye uhusiano mpya.

Vyanzo vinaeleza kuwa ingawa Britney anapenda kuwa kwenye mahusiano na angependa kupata mtoto wa kike siku za usoni, kwa sasa haoni haraka ya kuwa na mpenzi. Lengo lake kuu na kipaumbele chake kwa sasa ni kuendelea kujenga na kuimarisha upendo na uhusiano mzuri kati yake na wanawe.

CHANZO: US MAGAZINE

 

No comments