Watumiaji wa Microsoft wakumbwa na mkwamo wa seva

 



Kampuni kubwa ya teknolojia ya Microsoft inapambana kutatua hitilafu kubwa ya mifumo yake iliyoathiri makumi ya maelfu ya watumiaji kote duniani.

Huduma zilizoingia katika mgogoro ni pamoja na huduma Teams, Outlook pamoja na programu yake ya akili unde  ya Copilot.

Kwa mujibu wa shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, tatizo hilo lilisababishwa na baadhi ya seva kuzimika ghafla na kuongeza mzigo kwenye mifumo iliyobaki, jambo lililosababisha matatizo makubwa ya kuunganisha huduma hizo na kufanya watumiaji kushindwa kufikia baadhi ya nyaraka au taarifa za kalenda zao.

Mtandao wa ufuatiliaji wa Downdetector uliripoti kuwa malalamiko kuhusu Outlook pekee yalifikia karibu 140,000, ingawa taarifa zinaeleza kuwa hakuna dalili yoyote ya shambulio la mtandaoni kijiografia.



Imeelezwa na BBC kuwa athari za kushindwa kwa seva za Microsoft 365 zimesambaa hadi kwa makampuni mengine makubwa duniani, ikiwemo kampuni za akili unde ya OpenAI na Anthropic zinazotegemea miundombinu ya Microsoft, pamoja na makampuni mengine kama Workhorse Group yaliyolazimika kuahirisha ripoti zao za kifedha.

Licha ya Microsoft kueleza kuwa juhudi za kurejesha huduma zinaonyesha matokeo chanya, bado ilionya kuwa baadhi ya huduma zilizopatikana zinaweza kukata tena wakati wowote.

Watumiaji katika nchi mbalimbali kama Marekani, Japan na Singapore wanaendelea kukumbana na changamoto hizo wakati wahandisi wakifanya kazi usiku na mchana kurudisha hali ya kawaida.

 

No comments