TANZANIA NA UTURUKI KUKUZA BIASHARA, KUONGEZA USHIRIKIANO

 



Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji, zikilenga kuongeza thamani ya biashara baina yao kwa manufaa ya pande zote mbili.

Hayo yamefikiwa tarehe 12 Novemba, 2026, katika mazungumzo kati ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mheshimiwa Recep Tayyip ErdoÄŸan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki.

Marais hao wamekubaliana kuweka mazingira wezeshi na kuondoa vikwazo vya kibiashara vilivyosalia, pamoja na kupanua masoko ya bidhaa za kilimo na madini baina ya Tanzania na Uturuki.

Upatikanaji wa masoko hayo unalenga kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara wa pande zote mbili kunufaika zaidi na uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo, sambamba na juhudi za kuongeza thamani ya biashara.

Rais Dkt. Samia amehimiza wawekezaji wa Uturuki kuwekeza katika viwanda vya nguo, usindikaji wa chakula na uzalishaji vya vifaa vya ujenzi nchini, pamoja na kuhamisha teknolojia.

Amesema uwekezaji katika maeneo hayo unatarajia kuongeza uwezo wa uzalishaji nchini, kupanua shughuli za usindikaji na kufungua fursa za ajira kupitia ushirikiano wa viwanda kati ya Tanzania na Uturuki.



Viongozi hao pia wamejadili ushirikiano wa kuongeza fursa za masomo na mafunzo ya amali kwa wanafunzi wa Tanzania, ili kuendeleza ujuzi unaohitajika katika shughuli za uzalishaji nchini.

Katika eneo la uwekezaji, mazungumzo yamegusia hatua za utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Ofisi ya Rais ya Uwekezaji ya Uturuki.

Vilevile, wamejadili utekelezaji wa Mkataba wa Kuepusha Utozaji wa Kodi Mara Mbili, ambao ni miongoni mwa mikataba muhimu katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo.

Hatua zilizojadiliwa zinalenga kuendeleza utekelezaji wa makubaliano yaliyopo kati ya Tanzania na Uturuki na kupanua manufaa ya ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

No comments