COSOTA kugawa bilioni 1.3 kwa wasanii na Wabunifu

 


Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) inatarajia kugawa kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa wasanii na wabunifu nchini tarehe 26 Novemba mwaka huu.

Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa tozo ya hakimiliki ulioanzishwa kwa lengo la kuhakikisha wabunifu wananufaika kikamilifu na kazi zao za sanaa.

Ugawaji huo utafanyika jijini Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa tangazo lililotolewa awali mwezi Septemba na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki wa COSOTA, Naomi Mungure, ameeleza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 2.3 kuanzia mwezi Septemba 2023 hadi Juni 2026.

Kupitia kanuni za tozo hiyo, asilimia 60 ya fedha zilizokusanywa—ambayo ni sawa na shilingi bilioni 1.3—ndiyo itakayogawiwa moja kwa moja kwa walengwa.

Mungure alibainisha kuwa tozo hiyo ilianzishwa kufuatia maboresho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2022, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kulinda maslahi ya kiuchumi ya wasanii.

Ugawaji huu wa fedha unalenga kuboresha kipato cha wasanii na kuinua ubora wa kazi zao, ambapo makundi yatakayonufaika ni pamoja na wabunifu wa muziki, filamu, maandishi, sanaa za ufundi na sanaa za maonyesho.

Jumla ya aina 13 za vifaa vimeainishwa kutozwa tozo hiyo, ikiwemo CD, DVD, Digital Jukebox, MP3 Player, kadi za kumbukumbu (SD Card), Vinyl, Mini Disc, pamoja na redio na televisheni zenye uwezo wa kurekodi sauti na picha.

No comments