Nguvu ya Wanamichezo hakika ni Ufunguo wa Kujenga Maadili Katika Jamii Yetu




Tasnia ya michezo hapa nchini imezidi kujipambanua kuwa zaidi ya burudani ya dakika tisini au jukwaa la kushangilia ushindi na kushusha simanzi za matokeo. 

Katika jamii yetu ambapo mpira wa miguu na michezo mingine inaheshimika kama ibada ya pili, nguvu ya ushawishi waliyonayo wanamichezo wakubwa haiwezi kupimwa kwa mizani ya kawaida. Ni ukweli usiopingika kwamba mastaa hawa wa viwanjani wanatazamwa kama miungu wa kizazi cha sasa na vijana wetu kwani kila hatua wanayopiga, mtindo wa mavazi, na jinsi wanavyoishi vinageuka kuwa sheria ndogo ndogo zinazofuatwa na mamilioni ya vijana mitaani. Hali hii inawafanya wanamichezo kuwa na dhima kubwa ya kimaadili kuliko hata viongozi wengi wa kawaida, kwani sauti zao zinasikika na kupokelewa mara moja na roho za vijana wanaowapenda kwa dhati.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, alipokuwa akifungua mashindano ya hamsini na sita ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) mwaka 2026 yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, aligusa kidonda kilichopo wazi kwenye jamii yetu. 

Katika hotuba yake alitoa wito mzito uliowataka wanamichezo wenye majina makubwa kutumia nafasi zao za kipekee kuelimisha na kuhamasisha jamii kupinga mmomonyoko mkubwa wa maadili. Wito huu unakuja katika kipindi ambapo taifa linashuhudia wimbi la tabia zinazotishia misingi ya kitamaduni na kiroho ya kizazi kijacho. 

Dk. Nchemba alisisitiza kuwa jamii isipochukua hatua za makusudi mapema kukabiliana na changamoto hiyo, itajikuta kwenye lindi la madhara makubwa yatakayokuwa magumu mno kuyatengeneza baadaye, akifananisha mapambano haya na nguvu iliyotumika kupambana na dawa za kulevya au magonjwa hatarishi ya kuambukiza.

Umuhimu wa hoja hii kwa taifa letu ni mkubwa na haupaswi kupuuzwa kwa namna yoyote ile. Tanzania inaongozwa na nguvu kazi kubwa ya vijana ambao ndio wataalamu, viongozi, na wazazi wa kesho. Ikiwa mmomonyoko wa maadili utaachwa uendelee kutafuna misingi ya jamii yetu, nguvu kazi hiyo itapoteza mwelekeo na kuhatarisha mustakabali mzima wa nchi. 

Hivyo wanamichezo wanapojitokeza kukemea maovu, kuhimiza uaminifu, bidii, na staha, wanakuwa wanatumia jukwaa lao kujenga taifa lenye hofu ya Mungu na linalojitambua. Ni kama vile daktari anayetoa tiba sahihi kwenye kidonda kabla hakijasambaa mwilini kote. Ushawishi wa mwanamichezo unavuka mipaka ya viwanja vya mpira na kuingia moja kwa moja ndani ya nyoyo za mashabiki wao, jambo linalofanya ujumbe wao kuwa na nguvu ya kubadili mtazamo wa jamii kwa haraka kuliko mikutano mingi ya mihadhara ya kawaida.

Kwa nini hoja hii inaswihi hasa katika nchi yetu ambapo michezo mathalani soka ni kama ibada ya pili? Jibu ni rahisi na liko wazi mbele ya macho yetu kila siku. Hakuna taasisi nyingine hapa nchini inayoweza kukusanya watu wengi kwa wakati mmoja kama mpira wa miguu. Mashabiki wanatamani kuona kila kinachofanywa na wachezaji wao wanaowapenda. Wanapoteza sauti zao viwanjani wakishangilia, na wanatumia muda wao mwingi kujadili maisha ya mastaa hao mitandaoni na vijiweni. Hali hii inafanya michezo kuwa uwanja mzuri zaidi wa uhamasishaji.

Ikiwa mchezaji maarufu atapaza sauti yake na kukataa tabia chafu, au kuhimiza maadili mema, mashabiki wake watapokea ujumbe huo kwa hisia kali za kuamini na kuiga. Ni fursa ya dhahabu inayomilikiwa na taifa letu kugeuza shauku kubwa ya michezo kuwa silaha thabiti ya kulinda na kuimarisha utu na heshima ya Mtanzania.

Kiukweli wito wa Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba unapaswa kuchukuliwa kama mwongozo wa kitaifa na sio kama maneno ya kawaida ya ufunguzi wa mashindano. Ni wajibu wa taasisi za michezo, viongozi wa klabu, vyombo vya habari, na wanamichezo wenyewe kusimama kidete na kutambua uzito walionao mabegani mwao. 

Hakika michezo inapotumiwa kama chombo cha kujenga jamii yenye maadili, tunajihakikishia usalama wa kesho yetu na kuacha alama ya kudumu inayovuka mipaka ya ushindi wa makombe na medali za dhahabu. Ni wakati sasa wa kila mwanamichezo mwenye jina kubwa kujitazama kiooni na kutumia umaarufu wake kama nuru ya kuongoza jamii kwenye njia iliyonyooka.

No comments