DAA yaongeza kasi kupiga Vita dawa za kusisimua misuli
Chama cha Riadha Dar es
Salaam (DAA) kinaongeza juhudi za kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua
misuli (doping) kwa kuwapatia elimu wanariadha, makocha pamoja na wadau
mbalimbali wa michezo kuhusu madhara ya matumizi ya dawa hizo zilizopigwa marufuku.
Katika
kufanikisha mpango huo, DAA imeandaa kliniki maalum itakayofanyika Desemba 10
na 11 mwaka huu, ikishirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) pamoja na
udhamini kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Makamu
Mwenyekiti wa DAA, Elizabeth Tungaraza, ameeleza kuwa matumizi ya dawa za
kusisimua misuli sio suala dogo kwani yanaharibu sifa ya nchi, yanadhoofisha
maendeleo ya wanariadha na kuondoa imani kwenye michezo.
Alionya kuwa
wanamichezo wanaobainika kutumia dawa hizo wapo kwenye hatari ya kupoteza medali
na mataji, jambo linaloiletea nchi aibu kubwa.
Kliniki hiyo
inalenga kuongeza uelewa kuhusu vitu vilivyopigwa marufuku na itahusisha pia
waamuzi na waandishi wa habari ili wasaidie kueneza elimu ya michezo safi kwa
umma.
Wakati
huo huo, Katibu Mkuu wa DAA, Felix Chunga, amebainisha kuwa chama hicho
kinatarajia kushiriki katika mashindano ya riadha ya First Ladies
yatakayofanyika kuanzia Novemba 27 hadi 29 katika viwanja vya Shule ya Filbert
Bayi.
DAA inaendelea
kupanga shughuli zaidi za kukuza mchezo wa riadha mkoani humo na inawaomba
wadau mbalimbali kujitokeza kutoa ushirikiano ili kufanikisha malengo
yaliyowekwa.

Post a Comment