TANZANIA NA BENKI YA EXIM YA UTURUKI WAJADILI UFADHILI WA RELI YA SGR NA UKUAJI WA BIASHARA
Na Benny
Mwaipaja, Antalya-Uturuki
Serikali
ya Tanzania iko katika hatua za mwisho za mazungumzo na Benki ya Exim ya
Uturuki ili kupata ufadhili wa dola za Marekani milioni 280 kwa ajili ya
kukamilisha ujenzi wa kipande cha tatu na cha nne cha mradi wa reli ya kisasa
(SGR).
Mazungumzo
hayo yamefanyika Jijini Antalya nchini Uturuki, kando ya
Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu
Mabadiliko ya Tabianchi COP31, kati ya ujumbe wa Tanzania ukiogozwa na Waziri
wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar na Ujumbe wa Benki ya Exim ya Uturuki
ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Ali Guney.
Mhe.
Balozi Omar amesema kuwa ujenzi wa mradi huo wa kimkakati wa SGR kipande cha
tatu na nne wenye urefu wa zaidi ya kilometa 700, una thamani ya dola za
Marekani bilioni 1.6 ambapo kiasi cha dola bilioni 1.32 kimeshapatikana, na
kiasi cha dola milioni 280 ndicho kinachosubiriwa ili kukamilisha bajeti hiyo.
“SGR Ni mradi mkubwa
wa miundombinu unaochukua zaidi ya kilomita 2,000. unaolenga kuunganisha jiji
la bandari la Dar es Salaam kwenye pwani ya mashariki na mikoa ya magharibi ya
Mwanza na Kigoma hadi nchi jirani, ikiwemo Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo” amesema Mhe. Balozi Omar
Amesema kuwa Mradi huo umegawanywa
katika sehemu sita tofauti, zinazojulikana kama loti ambapo loti mbili za
kwanza, zinazounganisha Dar es Salaam na Mji Mkuu wa Serikali, Dodoma, tayari
zimekamilika na zinafanya kazi na kupokelewa vizuri na umma.
Amesema kuwa tofauti
na miradi mingi ya reli ya kikanda inayotegemea dizeli, reli ya Tanzania (SGR)
inatumia umeme, hatua inayoendana na ajenda ya Mkutano wa COP 31 unaofanyika
Antalya-Uturuki, unaohimiza matumizi ya nishati safi ili kutunza mazingira na
kuufanya mradi huo kuwa kielelezo endelevu cha usafiri wa kikanda.
Kwa ipande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Uturuki, Bw. Ali Guney, amesema kuwa
Benki yake inathamini ujenzi wa mradi huo kwa maendeleo ya Tanzania na nchi
jirani na kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo itakutana mwezi huu kujadili
maombi ya ufadhili huo unaohitajika ili kukamilisha ujenzi wa Reli hiyo ya
kisasa.
Bw. Guney
amesema kuwa licha ya ujenzi wa Reli, Benki yake inaangalia pia maeneo mengine
ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki katika nyanja za kiuchumi na
kibiashra, ufadhili wa miradi ya miundombinu ya baadaye, ikiwemo barabara na
madaraja, kama sehemu ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi.
Hatua hiyo
inaendana na malengo ya biashara kati ya nchi mbili yaliyowekwa
na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, na Mhe. Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki ambao
wamelenga ukuaji wa biashara kati ya Mataifa hayo mwili ufikie angalau dola za
Marekani bilioni moja.
Mwisho

Post a Comment