DKT. MWIGULU AZINDUA KITAMBULISHO CHA TAIFA KILICHOBORESHWA
=Serikali yawekeza zaidi ya Sh. bilioni 30 katika kadi na mashine za uzalishaji
=Asisitiza wananchi kupata vitambulisho bila usumbufu
=Vitambulisho vya awali vinaendelea kutumika
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua kitambulisho cha Taifa kilichoboreshwa, toleo la mwaka 2026, akisisitiza kuwa uwekezaji huo unapaswa kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza usumbufu kwa wananchi.
Katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Stendi ya Zamani ya Mailimoja, Kibaha, mkoani Pwani, Waziri Mkuu pia amezindua teknolojia mpya ya uzalishaji wa vitambulisho, programu tumizi ya NIDA Wallet na magari 10 ya huduma za usajili.
Amesema maboresho hayo yanafungua fursa ya kuunganisha huduma mbalimbali kupitia utambulisho mmoja, hivyo kupunguza ulazima wa wananchi kubeba vitambulisho vingi katika shughuli zao za kila siku.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha uwekezaji huu unaleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya kila siku ya Mtanzania,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa kila Mtanzania anayestahili kupata kitambulisho cha Taifa anapaswa kukipata kwa wakati, bila usumbufu wala urasimu.
Amempongeza Rais Dkt. Samia kwa kuwezesha uwekezaji huo, akisema matumizi ya teknolojia yanapaswa kuboresha huduma, kuimarisha utawala bora na kupanua fursa za wananchi katika shughuli za kiuchumi.
Akifafanua maboresho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, amesema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 30 katika ununuzi wa kadi mpya na mashine tano za kisasa zenye uwezo wa pamoja wa kuzalisha vitambulisho 2,800 kwa saa.
Amesema mashine hizo zinatumia teknolojia ya kuchora taarifa na picha kwa mionzi ya leza ndani ya tabaka za kadi, badala ya kuzichapisha kwa wino juu ya uso wake. Hatua hiyo inalenga kuongeza uimara wa kitambulisho na kupunguza uwezekano wa kughushi.
Aidha, amesema nafasi za programu za kidijitali zinazoweza kuunganishwa kwenye kadi zimeongezwa kutoka nne hadi nane, ili kuwezesha matumizi mapana zaidi ya kitambulisho hicho katika huduma mbalimbali.
Ameeleza kuwa uunganishaji wa huduma, zikiwemo bima ya afya, leseni za udereva na usafiri, utafanyika kwa hatua kulingana na utayari wa mifumo, makubaliano ya taasisi husika na matakwa ya kisheria.
“Lengo si kuongeza teknolojia kwa ajili ya teknolojia, bali ni kumwezesha mwananchi kutumia utambulisho wake katika huduma mbalimbali kwa usalama na urahisi zaidi,” amesema Kaji.
Kuhusu NIDA Wallet, amesema ni programu tumizi inayowezesha mwananchi kuwa na utambulisho wake wa kidijitali kwenye simu na kuutumia kuthibitisha taarifa zake wakati wa kupata huduma, kadiri mifumo ya taasisi husika itakavyounganishwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesisitiza kuwa uzinduzi huo hauondoi uhalali wa vitambulisho vya awali, hivyo wananchi hawalazimiki kubadilisha vitambulisho visivyo na dosari.
“Hauna sababu ya kwenda kubadilisha kitambulisho chako cha zamani kwenda kupata kipya kama hakuna sababu yoyote ya msingi,” amesema.
Katambi pia amewahimiza wananchi kuchukua vitambulisho vilivyo tayari katika maeneo walikojisajili.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Paschal Inyasi Chinyele, amepongeza maboresho hayo, huku akisisitiza ulinzi wa taarifa binafsi za wananchi, ushirikiano baina ya NIDA na taasisi nyingine na uendelevu wa teknolojia inayotumika.
Post a Comment