TANZANIA YASHIKA NAFASI YA TANO AFRIKA MAGEUZI UTAWALA BORA
Tanzania imeshika nafasi ya tano barani Afrika na ya 80 duniani katika Ripoti ya Fahirisi ya Utawala Bora ya Chandler (Chandler Good Government Index – CGGI) kwa mwaka 2026, inayotathmini uwezo na utendaji wa serikali kote ulimwenguni.
Ripoti hiyo iliyotolewa rasmi tarehe 22 Oktoba 2026 inaonyesha kuwa Tanzania imepata ongezeko kubwa zaidi la alama za jumla miongoni mwa nchi 23 za Afrika zilizofanyiwa tathmini mfululizo tangu kuanzishwa kwa fahirisi hiyo mwaka 2021, hatua inayodhihirisha maboresho makubwa katika mifumo ya uendeshaji wa shughuli za umma.
Maboresho makubwa zaidi kwa Tanzania yamejiri katika maeneo ya uundaji wa sheria na sera imara pamoja na ujenzi wa taasisi zenye nguvu.
Katika kipengele cha sheria na sera imara, Tanzania imeongoza barani Afrika kwa ongezeko la alama, huku nafasi yake duniani ikipanda kutoka ya 89 hadi ya 85.
Eneo la taasisi imara nalo lilionyesha ongezeko kubwa la alama nchini ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika, ingawa nafasi yake duniani katika kipengele hicho ilishuka kutoka ya 92 hadi ya 100 kutokana na nchi nyingine kupiga hatua kwa kasi zaidi katika utekelezaji wake.
Katika eneo la uongozi na maono ya baadaye, Tanzania imefanya mapinduzi makubwa kwenye kipengele cha ubunifu, ambapo imepaa kwa nafasi 40 duniani kutoka nafasi ya 83 hadi ya 43. Hata hivyo, tathmini hiyo imebainisha kuporomoka kwa alama za nchi katika maeneo ya usimamizi wa fedha, ushawishi, na sifa ya kimataifa, ikionyesha maeneo yanayohitaji marekebisho ya haraka.
Mkurugenzi wa Maarifa wa Chandler Governance Group, Dinesh Naidu, akizungumzia matokeo hayo alisema maendeleo yaliyopatikana katika sheria, sera na taasisi nchini Tanzania yanaashiria juhudi za dhati za kujenga taasisi zilizowazi na zenye ufanisi.
Alibainisha kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha mafanikio hayo yanaonekana pia katika maeneo mengine yanayopimwa na fahirisi hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa serikali kutumia takwimu na ushahidi kuweka vipaumbele vya mageuzi badala ya kuangalia nafasi katika orodha pekee.
Katika mchanganuo wa kikanda wa mwaka 2026, Mauritius imeongoza Afrika kwa kushika nafasi ya 55 duniani, ikifuatiwa na Rwanda (62), Botswana (70), Morocco (79), Tanzania (80), na Afrika Kusini inayofunga sita bora za Afrika ikiwa katika nafasi ya 85 duniani.
Kwa ujumla, nchi za Afrika zilionyesha maboresho ya wastani katika maeneo sita kati ya saba yanayopimwa, ingawa wastani wa bara zima bado upo chini ya kiwango cha mwaka 2021. Tathmini ya mwaka huu imehusisha nchi 133 duniani—zinazowakilisha asilimia 94 ya watu wote ulimwenguni—ikijumuisha nchi saba mpya za Afrika ambazo ni Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Gambia, Guinea, Lesotho, Liberia na Togo.
Fahirisi ya CGGI hutumia viashiria 35 vyenye uzito sawa vilivyogawanywa katika maeneo saba ili kusaidia serikali kutambua upungufu, kufuatilia maendeleo, na kujifunza kutoka kwa mataifa mengine.

Post a Comment