SERIKALI YAFUNGUA DIRISHA LA PILI LA MIKOPO KWA VIJANA



Serikali imetangaza rasmi kufunguliwa kwa awamu ya pili ya dirisha la mikopo kwa vijana nchini, huku ikiwasisitiza vijana wote kujitokeza kwa wingi na kujisajili katika Mfumo wa Uwezeshaji Vijana (YES) ili kupata fursa ya kunufaika na mikopo hiyo inayolenga kukuza uchumi na kubuni ajira.

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Kedmon Mapana, alitoa wito huo alipokuwa mkoani Mwanza wakati wa shughuli ya uvunaji wa samaki wa Kikundi cha Kitwima kilichopo Wilaya ya Nyamagana—kikundi kilichowezeshwa kwa mkopo wa Shilingi milioni 106 kupitia mfuko na programu ya mikopo ya Shilingi bilioni 200 chini ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya vijana.

Mapana alieleza kuwa serikali imeridhishwa na hatua kubwa iliyofikiwa na kikundi hicho cha vijana saba wasomi waliowekeza kwenye ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Victoria, akibainisha kuwa mfumo wa YES utaisaidia serikali kutambua maeneo walipo vijana, ujuzi wao, elimu zao na shughuli wanazozifanya ili kuwafikia kwa urahisi zaidi.

Kikundi hicho cha Kitwima kinatarajia kuvuna tani 15 za samaki kutoka katika vizimba vyake sita na kupata mapato ya zaidi ya Shilingi milioni 127 baada ya miezi sita hadi saba ya utekelezaji wa mradi huo, hatua iliyomfanya Mapana kuwahimiza kuongeza idadi ya vizimba kufikia kati ya 10 na 20 katika awamu inayofuata, huku akiahidi kuwa serikali itaunga mkono mpango wao wa kununua boti ya kisasa na kuwasisitiza kuomba mkopo mwingine pindi watakapokamilisha marejesho ya sasa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Viumbe Maji (Kitengo cha Maji Baridi) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Yohana Mirumbe, alibainisha kuwa matokeo hayo ni uthibitisho thabiti kuwa uchumi wa buluu una nafasi ya kipekee katika kubadilisha maisha ya vijana nchini. 

Wito huo uliungwa mkono na Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Mwanza, Diana Francis, aliyewataka vijana kushiriki kikamilifu kwenye majukwaa ya vijana ili kupata taarifa za fursa za mikopo, wakati Mkuu wa Biashara Changa na Uwezeshaji wa Benki ya CRDB, Fadhili Bushagana, akithibitisha kuwa benki hiyo inaendelea kutoa elimu ya fedha na mitaji kwa vijana.

Katibu wa Kikundi cha Kitwima, Bung’e Kwaangw, alieleza kuwa kikundi hicho kilianzishwa na vijana wasomi walioungana kutafuta fursa za kiuchumi ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, mfano unaodhihirisha jinsi uwezeshaji wa serikali unavyoweza kugeuza elimu na ubunifu kuwa ajira za uhakika na zenye tija kwa taifa.

No comments