Tume ya Madini yatakiwa kusimamia bei madini ya viwandani
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameitaka Tume ya Madini kusimamia kwa karibu utekelezaji wa bei elekezi za madini ya viwandani ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wananufaika na shughuli zao na kupata malipo yanayostahili.
Mavunde amesisitiza kuwa bei elekezi si jambo la hiari, bali ni muhimu katika kulinda maslahi ya wachimbaji wadogo na kuhakikisha wanapata manufaa stahiki kutokana na rasilimali wanazozalisha.
Akizungumza leo, Oktoba 26, 2026, wakati wa kikao na wadau wa madini ya viwandani kutoka mikoa mbalimbali nchini, Waziri Mavunde amesema sekta ya madini ikisimamiwa vizuri inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa taifa na kuongeza utajiri kwa Watanzania.
Aidha, amewahimiza wachimbaji wadogo wa madini ya viwandani kuunganisha nguvu na mitaji kwa kuanzisha viwanda vya uchakataji, hatua itakayoongeza thamani ya madini, kupanua fursa za ajira na kuongeza mapato yao.
Kuhusu utafiti wa madini, Mavunde amesema Serikali imeridhia kutenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na madini kwa ajili ya shughuli za utafiti, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa rasilimali zilizopo nchini na kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, amesema kutokana na kuwepo kwa tozo nyingi zinazokwamisha maendeleo ya wachimbaji, Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwa Wizara ya Madini, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Fedha kukutana ili kupitia tozo hizo na kubaini namna bora ya kuondoa zile zinazokwamisha shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amewahimiza wadau wa madini ya viwandani kuanzisha vyama vya ushirika ili kuimarisha biashara ya madini hayo, kuwaunganisha wachimbaji wadogo na kuongeza uwezo wao wa kiuchumi.
Amesema ushirika unaweza kuwawezesha wachimbaji kushirikiana katika mitaji na shughuli za kibiashara, pamoja na kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini ya ujenzi ili kurahisisha upatikanaji wa masoko na kuboresha biashara ya madini hayo nchini.

Post a Comment